Ilemela yataja siri kuongoza ufaulu shule za msingi, sekondari Mwanza

Mwanza. Uwepo wa lishe shuleni ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchochea kupanda kwa taaaluma katika shule za msingi na sekondari zilizoko Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.

Ilemela imeibuka kinara kitaaluma katika matokeo ya darasa la nne, saba, kidato cha pili na kidato cha nne ya mwaka 2024, mbele ya halmashauri nyingine saba za Mkoa huo ambazo ni Misungwi, Kwimba, Sengerema, Buchosa, Magu, Ukerewe na Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi Februari 20, 2025, na Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani humo, Sylvester Mrimi katika mkutano wa wadau wa elimu wilayani humo uliojadili mafanikio hayo na kuweka mkakati wa kuyaendeleza.

Hadi kufikia Desemba 2024, Halmashauri ilikuwa na jumla ya shule 57 kati ya hizo, shule 20 kati ya 33 za Serikali zinatoa chakula shuleni sawa na asilimia 60 huku shule 24 kati ya 24 za binafsi na mashirika ya dini nazo zikitoa huduma ya chakula sawa na asilimia 100.

Hivyo kwa ujumla wake, shule zinatoa chakula katika halmashauri hiyo ni asimilia 80.38 kwa wanafunzi wote wa Serikali na waliopo katika shule binafsi.

Mbali na uwepo wa lishe shuleni, Mrimi ametaja sababu nyingine zilizochochea Ilemela kuwa kinara kielimu kati ya halmashauri nane za mkoani humo, Mrimi ametaja motisha na ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za taaluma za watoto wao.

“Katika shule zetu za sekondari tumeweka motisha shule yoyote itakayopata ufaulu wa wastani wa daraja ‘A’ inapatiwa zawadi ya Sh3 milioni, pia kwa shule za itakayokuwa ya kwanza kumaliza wanafunzi wake wote wakifaulu mtihani wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) inapata Sh600,000,” amesema Mrimi.

Pia ametaja ufuatiliaji wa takwimu za mahudhurio ya wanafunzi shuleni kila mara kuwa umesaidia kupunguza uwepo wa utoro sugu shuleni ambapo takwimu zinaonyesha kwa mwaka 2024, idadi ya utoro sugu ilibainika kuwa ni wanafunzi 137 pekee,” amesema ofisa elimu huyo.

Kuhusu kidato cha kwanza, jumla ya wanafunzi 10,866 walichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za Manispaa hiyo mwaka 2025, ukilinganisha na wanafunzi 11,332 Januari, 2024.

Hadi kufikia Februari 14, 2025, wanafunzi 11,054 sawa na asilimia 101.7 walikuwa wameripoti na kuanza masomo yao jambo ambalo linaashiria kuwa na mwendelezo mzuri wa masomo yao. Wanafunzi 240 sawa na asilimia 2.2 bado hawajaripoti huku mkakati wa kuwasaka ukianza kutekelezwa.

Akigusia faida za kutoa lishe shuleni, Ofisa Elimu Awali na Msingi Halmashauri ya Manispaa hiyo, Mashelo Bahame amesema uwepo wa lishe shuleni unachochea mwanafunzi kupata muda wa kutosha kuhudhuria vipindi, kupunguza utoro na kuimarisha afya zao.

“Awali hali ilikuwa mbaya, ukifuatulia huko nyuma Halmashauri ya Ilemela ilikuwa inashika nafasi ya pili ama chini zaidi kitaaluma lakini katika kipindi cha mwaka mmoja wa kutoa huduma hii shuleni tumeona mabadiliko makubwa,” amesema.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mbunge wa Ilemela (CCM), mkoani humo, Angeline Mabula amesema utaratibu kutoa chakula shuleni siyo tu unamuongezea mwanafunzi umakini na utulivu darasani, pia unamuepusha dhidi ya hatari ya kuugua magonjwa ya mlipuko anayoweza kuyapata kwa kula chakula mtaani kiholela.

“Huu ni mkakati ambao naamini hata Halmashauri nyingine zikiiga, basi si ajabu wanafunzi watafanya vizuri darasani na itawezesha kupaisha ufaulu wao darasani na kukuza taaluma kuanzia elimu msingi hadi sekondari,” amesema Mabula.

Awali, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ilemela mkoani humo, Hassan Masala ametaja changamoto ambazo bado zinaendelea kuikumba Halmashauri hiyo kuwa ni pamoja na uhaba wa miundombinu ya kujifunzia ikiwemo madarasa na madawati huku akitaja mikakati ya kuzitatua.

DC Masala amesema uhitaji wa vyumba vya madarasa Ilemela katika shule za msingi na sekondari ni vyumba vya 1, 518 vya madarasa, vilivyopo ni 768 huku kukiwa na upungufu wa vyumba 750 jambo ambalo linasababisha msongamano wa wanafunzi darasani katika baadhi ya shule.

Pia amesema mahitaji ya madawati kwa shule za msingi na Sekondari za Ilemela ni madawati 28,184, yaliyopo (22,495) huku kukiwa na upungufu wa madawati 5,689 jambo ambalo limesababisha baadhi ya wanafunzi katika shule (bila kuzitaja) kulazimika kukaa zaidi ya idadi inayohitajika.

“Uwepo wa elimu bure umeongeza hamasa ya wananchi kupeleka watoto wao shuleni kiasi kwamba kuna wakati wanafunzi wanakuwa wengi kuliko miundombinu. Serikali tumeanza utengenezaji wa madawati kwa kutumia fedha za makusanyo ya ndani ya halmshauri na wadau tuondoe changamoto hiyo,” amesema Masala.

Hata hivyo, Masala amesema Serikali wilayani humo kwa kushirikiana na wadau wa elimu tayari wameanzisha mkakati wa kutengeneza madawati 17,500 katika mwaka wa fedha 2024/26, ili kumaliza uhaba huo na tayari madawati zaidi ya 1,420 yameshatengezwa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani humo, Ummy Wayayu amesema Halmashauri hiyo itatenga fedha katika makusanyo yake ya ndani (bila kuitaja) kwa ajili ya kupunguza changamoto za kujifunzia ili kuifanya Ilemela kuendelea kuwa kinara kitaaluma kimkoa na kitaifa.

“Tunapikusanya tunahakikisha tunatenga asilimia kadhaa ya fedha za ndani kusaidia kuimarisha miundombinu ya elimu katika Wilaya yetu. Lengo ni kuhakikisha watoto wetu wanasoma katika mazingira mazuri bila kikwazo chochote,” amesema Wayayu.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Jeshini iliyopo katika halmashauri hiyo, Arafa Lema amesema uboreshaji wa miundombinu na utoaji wa lishe shuleni umewapunguzia walimu kazi ya kuwatuliza wanafunzi darasani.

“Zamani watoto walikuwa hawatulii darasani kwa sababu ya njaa, lakini sasahivi wanapata muda wa kutosha kufundishwa na kujifunza. Hata sisi walimu tunapata utulivu na muda wa kutosha kuwafundisha wakatuelewa,” amesema mwalimu, Arafa.

Mkazi wa Kijiji na Kata ya Kayenze wilayani humo, Josiah John amesema changamoto katika Sekta hiyo haziwezi kumalizwa huku akiipongeza Serikali kwa kujitahidi kuhamasisha wananchi kuwa sehemu ya kutatua changamoto za kielimu katika Halmashauri hiyo.

Mbali na kujadili mkakati wa kuendeleza ufaulu huo kitaalum, Mkutano wa leo umeambatana na utoaji wa zawadi na vyeti kwa walimu waliofanya vizuri katika masomo yao sambamba na watumishi wa Halmashauri waliochochea kupaa kwa ufaulu huo.

Related Posts