Kuna nini Yanga? Mwingine asepa!

ALIANZA aliyekuwa kocha mkuu, Sead Ramovic, kisha akafuata kocha wa makipa Alaa Meskini, kiasi cha kuanza kuzua maswali, Yanga kunani?

Ndio, Ramovic aliyeajiriwa na Yanga, Novemba 15 mwaka jana kuchukua nafasi ya Miguel Gamondi, alitangaza kuondoka Jangwani Februari 5 mwaka huu na wiki mbili tu, Meskini naye aliomba kuondoka, lakini mapema leo taarifa nyingine imetoka.

Siku chache tu tangu aliyekuwa kocha wa makipa wa Yanga, Alaa Meskini raia wa Morocco kuondoka, kocha mwingine wa mazoezi ya viungo wa timu hiyo, Adnan Behlulovic amedaiwa ameondoka katika timu hiyo ikielezwa anaenda kuungana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Saed Ramovic.

Ramovic kwa sasa yupo CR Belouizdad ya Algeria na ndiye aliyemleta kocha huyo wakati timu ikiwa katika michuano ya kimataifa na inaelezwa Behlulovic anamfuata huko.

Mwanaspoti lilimtafuta kocha huyo kufahamu nini sababu iliyoamua kumuondoa hakutaka kuweka wazi huku akisisitiza ameondojka kwa makubaliano baina yake na Yanga.

“Napenda kutoa shukrani kwa viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wote tulikuwa na wakati mzuri sana bila kusahau mashabiki wamenionyesha upendo nilijiona nipo nyumbani wakati wote tutaonana wakati mwingine,” alisema huku akisita kuweka wazi sababu iliyo muondoa.

Huyu ni kocha wa pili mfululuzo kuondoka baada ya Meskini tangu Ramovic alipoondoka kwenda CR Belouizdad na kocha huyo wa makipa ametua FAR Rabat ya Morocco.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga, kimeliambia Mwanaspoti siku chache baada ya Meskini, Behlulovic ambaye alijiunga na Yanga chini ya Ramovic pia ameomba kuondoka na tayari amewaaga wachezaji.

“Kwa upande wa Meskini nafikiri sababu iliwekwa wazi lakini kwa huyu hadi sasa sijapata sababu maalum iliyomfanya afanye uamuzi huo aliouchukua ninachoweza kusema ni amewaaga wachezaji kuwa hatakuwa sehemu ya kikosi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Tunasubiri taarifa ya viongozi kuhusiana na uamuzi huo wa makocha wawili kuondoka kwa wakati mmoja na timu ikiwa bado inaendelea na mashindano japo kuna sababu zinatajwa kuwa mabadiliko ya benchi la ufundi yanaweza kuwa sababu ya kuondoka kwake.”

Kocha huyo ambaye ni raia wa Bosnia-Herzegovina alichukua nafasi Taibi Lagrouni ambaye uongozi hakumuondoa kikosini huenda akarudishwa kwenye nafasi hiyo ili kuendelea na majukumu kwa kipindi hiki.

Wawili hao walikuwa wanafanya kazi pamoja kabla ya mmoja ambaye ameingia kati kati ya msimu kuamua kuchukua uamuzi wa kuondoka mwenyewe kikosini bila ya kuweka wazi sababu.

Related Posts