KIKOSI cha Simba jana jioni kilikuwa uwanjani kuvaana na Namungo katika mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini leo masikio na macho itakaelekeza mjini Doha, Qatar kwa ajili ya kufuatilia droo ya mechi za robo fainali ya michuano ya CAF, huku ikiwa na kazi ya kujipanga kukabiliana na timu yoyote itakayopewa.
Simba ilimaliza kinara wa Kundi A kwa kuvuna pointi 13 mbele ya CS Constantine ya Algeria iliyomaliza ya pili na alama 12, wakati Bravos do Maquis ya Angola ikiwa ya tatu na pointi saba na CS Sfaxien ya Tunisi ikishika mkia katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na leo droo yake inafanyika Qatar.
Huu ni msimu wa sita kati ya saba kwa Simba kufika robo fainali ya michuano ya CAF tangu iliporejea kimataifa msimu wa 2018-2019 na kuna uwezekano wa kukutana ama na Al Masry ya Misri au ASEC Mimosas ya Ivory Coast ama Stellenbosch ya Afrika Kusini.
Stellenbosch ni wageni katika michuano ya CAF na haijawahi kabisa kukutana na Simba, lakini rekosi zao zinatoa picha kwamba Wekundu wanapaswa kujipanga iwapo watangukia mikononi mwa timu hiyo ya Sauzi, iwapo inataka kurejea rekodi ya kufika nusu fainali ya michuano hiyo baada ya ile ya 1974.
Simba ilifika hatua hiyo mwaka huo wakati michuano hiyo ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika na kutolewa kwa penalti na Ghazl El Mahalla ya Misri bada ya kila mmoja kushinda nyumbani kwa bao 1-0.
Kwa timu za Asec na Al Masry sio wageni kwa Simba kwani zilishacheza nao katika hatua tofauti za michuano ya CAF, lakini Wekundu wanapaswa kutafuta mbinu mpya za kuweza kutoboa mbele ya wapinzani wao hao kama mmoja anaangukia mikononi mwao baada ya ya droo ya leo.
Simba ilishawahi kukutana na Al Masry katika raundi ya pili y Kombe la Shirikisho 2018 na ikang’olewa kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya 2-2 Kwa Mkapa na kwenda kuambulia suluhu ugenini.
Kwa ASEC ni moja ya timu iliyokutana nao mara nyingi katika michuano ya CAF ikicheza hatua ya makundi misimu mitatu tofauti, mbili zikiwa za Ligi ya Mabingwa 2003 na 2023-2024 na Kombe la Shirikisho 2021-2022 na hakuna mbabe baina yao kwa matokeo ya jumla, kwani kila timu imeshinda mechi mbili ikiwa nyumbani na kupoteza mbili pia za ugenini na nyingine mbili kuisha kwa sare.
2003 zikiwa kundi moja katika Ligi ya Mabingwa Simba ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 nyumbani na kufumuliwa 4-3 ugenini kisha kukutana tena 2022 katika Kombe la Shirikisho ambapo S8imba ilishinda nyumbani 3-1 na kulala ugenini 3-0 na msimu uliopita zikiwa tena katika kundi la Ligi ya Mabingwa, Simba ililazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na kwenda kutoka suluhu ugenini.
Kwa rekodi zilivyo kwa timu zote tatu ambazo moja inaweza kukutana na Simba ni dhahiri Wekundu wanapaswa kujipanga kama inataka kufika mbali msimu huu baada ya kukwamia hatua ya robo kwa misimi mitano iliyopita, ikiwamo minne ya Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho.
Hata hivyo, Stellenbosch inayonolewa na Kocha Mkuu, Steve Barker na inayoshiriki michuano hii kwa mara ya kwanza katika historia yake, inaweza ikawa faida kwa Simba ambayo imekuwa na uzoefu mkubwa, japo inapaswa kujipanga ili kutinga nusu fainali kama itajipanga mapema kabla ya kuikabili.
Timu hii ilifuzu michuano hii baada ya kutwaa taji la Carling Knockout Cup huko Afrika Kusini huku ikiwa tishio baada ya kuzifunga timu mbalimbali maarufu zikiwemo za Orlando Pirates, Chippa United na Amazulu ambazo zimejizoelea umaarufu.
Ikiwa Simba itapangiwa na Stellenbosch FC, itakuwa mara ya pili kwa siku za karibuni kukutana na timu kutoka Sauzi, baada ya msimu wa 2021-2022 pia katika Kombe la Shirikisho ilikutana na Orlando Pirates na kutolewa kwa penalti, lakini ilishawahi kucheza na Kaizer Chiefs katika Ligi ya Mabingwa na kutolewa robo kwa matokeo ya jumla ya 4-3. Simba ikilala ugenini 4-0 na kushinda nyumbani 3-0.
Kwa Al Masry ya Misri iliyomaliza nafasi ya pili ya Kundi D nyuma ya watetezi wa taji, Zamalek pia ya Misri waliotwaa msimu uliopita.
Kitendo cha Al Masry kumaliza nafasi ya pili kinaweza kuifanya kukutana na Simba ambapo ikiwa zitakutana itakuwa ni kwa mara ya tatu kwao katika michuano ya kimataifa kwa miaka ya hivi karibuni, baada ya miamba hiyo kukutana pia mwaka 2018.
Timu hizo zilikutana raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo mechi ya jijini Dar es Salaam zilitoka sare ya mabao 2-2, Machi 7, 2018, kisha marudiano Misri zikatoka suluhu (0-0), Machi 17, 2018, na Simba kutolewa kwa mabao ya ugenini.
Moja ya faida kubwa kwa Simba ni kumaliza kinara ambapo hatua ya robo fainali itaanzia ugenini na kumalizia nyumbani kwa mujibu wa kanuni ya 3(24), inayofafanua, “Washindi wa pili watacheza mechi zao za kwanza za robo fainali nyumbani.”
Faida nyingine kwa Simba ni kukutana na timu ambazo sio ngeni kwao na hazijawahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo tofauti na ilivyokuwa kwa vigogo vingine wakiwemo mabingwa watetezi Zamalek na USM Alger zote za Misri na RS Berkane ya Morocco.
Simba imetinga hatua ya robo fainali kwa msimu wa sita kati ya saba katika ushiriki wa michuano ya CAF tangu mwaka 2018, ikiwemo mbili ya Shirikisho Afrika na nne ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikiwa kinara wa kundi kwa mara yake ya pili.
Mara ya kwanza Simba kuongoza kundi tangu kipindi hicho ilikuwa msimu wa 2020-2021, iliposhiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kumaliza kinara wa kundi A na pointi zake 13, ikifuatiwa na Al Ahly ya Misri iliyomaliza ya pili na pointi 11.
AS Vita Club ya DR Congo ilimaliza ya tatu na pointi saba, huku Al Merrikh ya Sudan ikiburuza mkiani na pointi mbili tu, ambapo msimu huo Simba iliishia robo fainali baada ya kutolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-3.
Hatua ya Simba kutinga robo fainali kumeihakikishia timu hiyo kuvuna Dola 550,000 ikiwa ni zaidi ya Sh 1.4 bilioni na kama itavuka hapo na kutinga nusu itavuna Dola 750,000 (karibu Sh2 milioni).
Droo nyingine itakuwa ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ambapo mabingwa wa kihistori wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri iliyomaliza nafasi ya pili na pointi zake 10 katika kundi C, itafahamu mpinzani itakayokutana naye kwenye hatua hiyo.
Al Ahly ilimaliza nafasi hiyo nyuma ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini iliyomaliza na pointi 14, ambapo itakutana na kati ya Al Hilal (Sudan) iliyoongoza kundi A, AS FAR Rabat (Morocco) kundi B na Esperance ya Tunisia kutoka kundi D.
MC Alger ya Algeria iliyoibania Yanga mchezo wa mwisho na kumaliza nafasi ya pili kundi A, inaweza kukutana na AS FAR Rabat (Morocco) kundi B, Orlando Pirates ya Afrika Kusini kutoka kundi C na Esperance ya Tunisia kutoka kundi la D.
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyomaliza nafasi ya pili kundi B na pointi tisa, inaweza kukutana na ndugu zao wa Orlando Pirates kutokea kundi C, Al Hilal ya Sudan na Esperance ya Tunisia iliyomaliza kinara wa kundi D na pointi 13.
Pyramids iliyomaliza nafasi ya pili kundi D na pointi 13, sawa na Esperance ila zikitofautiana tu mabao ya kufunga na kufungwa, itakutana na kati ya Al Hilal (Sudan), AS FAR Rabat (Morocco) au Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Staa wa zamani wa soka barani Afrika na Algeria, Rabah Madjer atakuwa miongoni mwa watu maarufu watakaokuwa pamoja na Ofisa Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, atakayeambatana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu, Zubeda Sakuru.
Wawili hao ni miongoni mwa watu ambao wamealikwa kushiriki matukio mawili makubwa yatakayofanywa na Shirikisho la Mpira wa miguu Afrika (CAF), katika droo hiyo itakayofanyika makao makuu ya kituo cha runinga cha Bein Sports kuanzia saa 11 jioni.
Madjer atakayechezesha droo hiyo atashirikiana na nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Zambia, Rainford Kalaba mwenye historia kubwa na mashindano hayo yote mawili, kwani ameshayachukua kwa nyakati tofauti akiwa na TP Mazembe ya DR Congo.
WAKATI hali ikiwa si shwari kwa kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra kutokana na kufungwa mabao mepesi hivi karibuni yanayoonekana yanatokana na makosa binafsi, kocha aliyekuwa akimnoa ndani ya timu hiyo ameomba kuondoka na taarifa zinasema tayari ametoa FAR Rabat ya Morocco.
Kocha huyo anayemnoa Diarra na makipa wengine katika kikosi cha Yanga, alikuwa ni Alaa Meskini raia wa Morocco ambaye ameuomba uongozi kumvunja mkataba wa kuendelea kuinoa kutokana na sababu za kifamilia na tayari jamaa ameshatimka Jangwani na kuibukia FAR Rabat iliyopo nchi anayotokea.
Kabla ya Diarra kuyumba hivi karibuni, kipa huyo wa kimataifa kutoka Mali alikuwa na mitatu mfululizo iliyopita ya mafanikio ikiwamo kutwaa tuzo mbili za Kipa Bora wa Ligi Kuu na moja ya Kombe la Shirikisho.
Makali ya Diarra yameonekana kupungua makali tofautio na alivyoanza msimu wa 2021-2022 alipotua Yanga, akitokea Stade Malien ya Mali ambapo msimu huo alitwaa tuzo ya Kipa Bora na kurudia tena na 2022-2023 alibeba tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu Bara na msimu uliopita alinyakua Kombe la Shirikisho.
Hata hivyo, wakati kipa huyo akijitafuta, huku akiacha maswali mengi kwa mashabiki waliofikia hatua ya kumbatiza jina la ‘Screen Protector’, taarifa kutoka ndani ya Yanga, zinabainisha kocha Meskini tayari ameandika barua ya kuvunja mkataba huku uongozi ukiridhia.
Mtoa taarifa huyo ameenda mbali zaidi na kutaja sababu ya kocha huyo kufikia uamuzi huo ni kuwa, anataka kuwa karibu na familia yake iliyopo Rabat, Morocco na Mwanaspoti limepenyezewa kuwa amejiunga na FAR Rabat inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco, Batola Pro.
“Kocha Alaa Meskini ameomba kuvunja mkataba na uongozi umeridhia kutokana na sababu alizozitaja, ambazo ni kuhitaji kuwa karibu na familia yake huko kwao Morocco.
“Amesema kwa sasa mama yake anaumwa na hakuna wa kumuuguza, anataka awe karibu naye ukizingatia kwamba hivi karibuni alifiwa na baba yake mzazi,” kilisema chanzo hicho.
Kocha Meskini aliyejiunga na Yanga Agosti 2023 wakati wa kocha Miguel Gamondi na hadi anaondoka Yanga tayari amefanya kazi na makocha watatu.
Mbali na Gamondi, kocha Meskini amefanya kazi na Sead Ramovic na Miloud Hamdi na hadi anaondoka alikuwa amebakiza mkataba wa miezi minne kabla ya kumalizika Juni 2025, huku Yanga ikiwa imecheza mechi 20 za Ligi Kuu Bara msimu huu ikifungwa mabao tisa na kimataifa iliruhusu sita katika mechi nane zikiwamo za raundi ya awali na zile za makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika.