Morogoro/Arusha. Wakati Jeshi la Polisi likiwashikilia watu 12 mikoa ya Mbeya na Morogoro, kwa tuhuma za kuendesha biashara ya fedha mtandaoni bila kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Serikali imezindua kampeni maalumu ya kudhibiti vitendo vya kitapeli na ulaghai.
Kampeni hiyo ya ‘Sitapeliki’ inalenga kutoa elimu kwa umma na kushughulikia masuala ya utapeli na ulaghai mitandaoni.
Pia, itatumika kuongeza uelewa wa mbinu zinazotumiwa na matapeli wa mtandaoni na kuwapa taarifa jinsi ya kujikinga na majaribio ya ulaghai yanayofanywa na watu wachache wenye lengo la kujinufaisha.
Kampeni hiyo imezinduliwa wakati kuna wimbi la watu kutapeliwa mitandaoni huku BoT ikipiga marufuku kwa wanaoendesha michezo hiyo bila leseni kwamba, hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Kampeni hiyo imezinduliwa leo Alhamisi, Februari 20, 2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa wakati wa kikao kazi kati ya Serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano kilichofanyika jijini Arusha.
“Kampeni hii ya Sitapeliko inalenga kutoa elimu kwa jamii kuchukua hatua mahsusi na jumbe mbalimbali zitasambazwa na kuepukana na utapeli mtandaoni,” amesema Silaa.
“Utapeli unahujumu mikakati ya Serikali kuendeleza ushirikishwaji wa wananchi kwenye mifumo ya kifedha na kujenga uchumi wa kidijitali. Ni matumaini yangu baada ya kuzindua kampeni hii, kila mdau atakwenda kutekeleza kwa wakati mpango huu utakaofanikisha lengo la kupeleka elimu na uelewa katika jamii juu ya kujikinga dhidi ya vitendo hivi,” amesema Silaa.
“Usalama na uimara wa mitandao unaongeza imani ya wananchi kutumia mifumo ya Tehama, inayochochea ushiriki wao kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.”
Akizungumzia kikao kazi hicho, ametaja mafanikio yaliyofikiwa katika sekta hiyo kuwa ni ufikishwaji wa mawasiliano ya mkongo wa Taifa katika wilaya 109 hati ya 139 nchini sawa na asilimia 78.
Amesema hadi kufikia Desemba 2024 kadi za simu za mkononi zilizosajiliwa ni milioni 86.8 hivyo kuwezesha Serikali kukusanya mapato kutokana na huduma za kidijitali.
Awali, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mohammed Abdulla amesema kikao kazi hicho kimelenga kutathimini utekelezaji wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa miaka 10 kuanzia 2024 hadi 2034.
Amesema mkakati huo utakuwa na nguzo sita za kuwezesha miundombinu ya kidijitali, utawala na mazingira wezeshi, uelewa wa kidijitali na maendeleo ya ujuzi, utamaduni wa ubunifu wa kidijitali na teknolojia wezeshi.
Nyingine ni kukuza ushirikishwaji wa kidijitali na ufikaji wa huduma za kifedha za kidijitali.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro na Mbeya limewashikilia watu 12 kwa tuhuma za kuendesha biashara ya fedha kwa njia ya mtandao bila kibali BoT.
Watuhumiwa hao saba kutoka Morogoro na watano Mbeya ni wawakilishi wa Kampuni ya Leo Beneth London (LBL).

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Alex Mkama
Akizungumza leo Alhamisi Februari 21, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema watuhumiwa hao walikamatwa Februari 18, 2025 eneo la Kirakala, Manispaa ya Morogoro, wakiwa na vifaa vinavyohusiana na biashara hiyo.
Watuhumiwa hao wakazi wa Morogoro ni David Francis (35) ambaye mkurugenzi wa kampuni hiyo, Boazi Amboniye (42) na mkurugenzi wa kampuni hiyo Tawi la Turiani, Kundi Msalaba (31).
Mwingine ni mhasibu wa kampuni hiyo, Moses Dugomela (22), mshauri wa kisheria wa kampuni hiyo, Isaya Paulo (25) na Baraka Sanga (32).
Amedai kuwa, pia wamemkamata Jackson John (30) akiwa amekusanya watu zaidi ya 30 ndani ya nyumba aliyokuwa akitumia kufanyia utapeli huo akiwa amewatoza watu hao Sh23 milioni.
Amesema msako huo umefanyika kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na BoT wilaya za Morogoro Mjini na Mvomero, kama sehemu ya kukabiliana na utapeli wa fedha kupitia mitandao ya simu na teknolojia nyingine za fedha.
Mmoja wa walioshiriki biashara hiyo, Thadei Hafigwa amesema alijiunga kupitia kiunganishi maalumu kwa gharama ya Sh50,000 na baada ya kujiunga aliletewa orodha ya video alizotakiwa kuzicheza kila siku na alikuwa akilipwa.
“Nimejiunga juzi tu, hata gharama za kujiunga hazijarudi lakini tunashukuru Jeshi la Polisi kwa kuwakamata wahusika wa kampuni hiyo,” amesema Hafigwa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ,Wilbert Siwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.Picha na Hawa Mathias
Katika hatua nyingine, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Wilbert Siwa amesema watu watano wamekamatwa eneo la Mwanjelwa kwa tuhuma za kuendesha biashara hiyo.
Amesema hayo leo Alhamisi Februari 20, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Watuhumiwa hao ni meneja wa kampuni hiyo ya LBL, Gerald Masanya (31), Saphina Mwamwezi (23), Edda William (29) Yohana Mkinda (29) nas Macrine Sinkala (23).
Amesema walipata taarifa za uwepo wa kampuni hiyo jana Jumatano na kufuatilia kwa kushirikiana na maofisa wa BoT.
“Tulifika maeneo ya Mwanjelwa karibu na duka la nguo liitwalo Vunjabei zilipo ofisi za kampuni hiyo tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano akiwamo meneja wa kampuni hiyo.
“Watuhumiwa wamekiri kupitia kampuni hiyo wamekuwa wakijihusisha na biashara ya upatu mtandaoni na kueleza wamekuwa wakitumia kiungo maalumu ‘link’ kwa wateja kujiunga mtandaoni.
“Wateja wakijiunga hutakiwa kulipa fedha kuanzia Sh50,000 mpaka 540,000 kwa kuangalia matangazo ya picha mbalimbali zilizowekwa kwa madai watapata faida kwa muda Fulani, baada ya kuwekeza fedha zao,”amesema kamanda.
Meneja uendeshaji wa BoT, Graciana Bemei amesema mtu yeyote anayefanya biashara bila leseni ni kosa la kifungu cha sheria 14, mfumo wa malipo ya fedha ya mwaka 2015.
Ametaja kifungu kingine cha sheria ya 12 cha utakatishaji fedha cha mwaka 2022 kama kampuni ikiendesha biashara bila leseni ya BoT itawabana katika sharia ya utakatishaji wa fedha.
Baadhi ya wachezaji wa mchezo huo wa LBL, John Frank si jina halisi mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam, amesema, “wanasema ni kampuni ya kimataifa imeingia ubia na kampuni kubwa za filamu duniani kama Paramount, 20th Century Fox, MGM Picture, Warner Brothers, Destiny, Dream Works Picture kwa kufanya matangazo ya movies kupitia kutazama trailers na kwamba, wao wanalipwa na kampuni na wao wanalipa watazamaji na ili unufaike lazima uweke fedha kupitia levels.
“P1-Level unaweka Sh50,000 unapewa trailers tano za kuangalia kupitia website yao kila trailer unalipwa Sh335, na kwa siku unalipwa Sh1,675 kwa mwezi 50,250,”amesema.
“P2 level unaweka Sh150,000, level nyingine unaweka Sh540,000, unapewa trailers 15 za kuangalia, kila trailer unalipwa Sh1200, kwa siku unalipwa 18,000, kwa mwezi unalipwa Sh540,000.”
Amesema kila unapokwenda hatua ya juu, ndio unaona faida inakuwa kubwa zaidi, hivyo watu wanachezewa kisaikolojia kwa wanaopenda maisha ya mkato.
“Kwanza ili utoe fedha zako unazolipwa lazima fedha hiyo, malimbikizo yake yafike Sh100,000 ndio utoe. Wanaamini kuna watu wenye tamaa wataweka fedha nyingi sana,” amesema.
Hairati Mzeru, mkazi wa Kimara Bonyokwa Dar es Salaam amesema amejiunga kwenye mchezo huo kwa Sh50,000, lakini hadi sasa hakuna kiasi kilichoongezeka kwenye akaunti yake.
“Walituambia kama unajiunga kwa hela kubwa basi ndivyo utakapopata hela nyingi, nilijiunga kwa Sh50,000 lakini hadi sasa sioni hela kuongezeka,” amesema Hairati.
“Baada ya kuona hela haiongezeki nikataka kujitoa ndipo nilipoambiwa hela yako hairudishwi, nikashtuka na kuona hapa naibiwa,” amesema.
Imeandikwa na Jackson John (Morogoro), Janeth Mushi (Arusha), Hawa Mathias (Mbeya)