Mfanyabiashara kortini wakidaiwa kukutwa na kemikali za vileo

Moshi. Mfanyabiashara Novita Shirima (49), mkazi wa Katanini na Dereva Justine Mbise (29), mkazi wa Bomambizi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi wakikabiliwa na mashtaka sita, ikiwemo kumiliki kemikali, inayotumika kutengeneza vileo aina ya ethanol kinyume cha sheria.

Pia, wanadaiwa kughushi stempu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kutumia nembo bandia za bidhaa zinazozalishwa na kampuni za vileo.

Shauri hilo limefikishwa mahakamani Jumatano, Februari 19, 2025, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Moshi, Ruth Mkisi.

Upande wa mashtaka unaongozwa na Wakili wa Serikali Frank Wambura, huku washtakiwa wakitetewa na Mawakili wawili, Emanuel Anthony pamoja na Marry Kway.

Akiwasomea mashtaka hayo, Wakili Wambura alidai kuwa mnamo Oktoba 10, 2024, katika Mtaa wa Katanini, mshtakiwa wa kwanza, Novita Shirima, alikamatwa akiwa na lita 310 za ethanol zinazodaiwa kutumika kutengeneza pombe bandia.

Mashtaka mengine yanawahusisha washtakiwa hao kwa pamoja, yakiwa ni ya matumizi haramu ya alama za biashara.

Novita Shirima pia anadaiwa kukutwa na stempu bandia za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na chapa za kughushi za bidhaa mbalimbali za vileo.

Wakili Wambura alieleza kuwa mnamo Oktoba 10, 2024, mshtakiwa huyo alikutwa na chupa 42 za mililita 750 zenye nembo bandia ya K-Vant, pamoja na chupa 144 za mililita 750 zenye nembo ya Konyagi. Kadhalika, inadaiwa kuwa alighushi alama za biashara kwenye chupa 182 za mililita 250 za pombe inayozalishwa na kampuni ya Highlife.

Washtakiwa hao walikana mashtaka yote yanayowakabili mahakamani hapo.

Upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika, hivyo uliomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo, huku ukiwasilisha hoja ya kuendelea kushikiliwa kwa watuhumiwa hao kwa kuwa makosa hayo hayana dhamana.

Baada ya hoja hiyo, pande zote ziliingia kwenye mabishano ya kisheria, ambapo Wakili Emanuel Anthony alisema wateja wake wanayo haki ya kupata dhamana, akirejea sehemu ya vifungu vya sheria inayohusika na dawa za kulevya.

Wakili Anthony alibainisha kuwa makosa ya washtakiwa yanaruhusu dhamana, lakini mahakama inapaswa kuwa na ushahidi wa kutosha iwapo kuna uhusiano wowote wa kesi hiyo na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Wambura akijibu hoja hizo, alieleza kuwa umiliki wa chini ya lita 30 za ethanol unaweza kupewa dhamana, lakini kwa zaidi ya kiwango hicho, dhamana haiwezi kutolewa.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mkisi aliahirisha shauri hilo kwa muda ili kupitia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili, pamoja na kupitia sheria husika.

Baadaye, Hakimu baada ya kusoma vifungu vya sheria na kulinganisha na hoja zilizowasilishwa, alieleza kuwa dhamana kwa washtakiwa iko wazi, huku akiweka masharti ya upatikanaji wa dhamana hizo.

Masharti hayo ni pamoja na washtakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa Serikali, kuweka dhamana ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh10 milioni kwa kila mmoja, na dhamana ya kiwanja kisichopungua thamani ya Sh100 milioni kikiwa katika eneo la Wilaya ya Moshi.

Sharti jingine ni kuwa washtakiwa hawataruhusiwa kusafiri nje ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Machi 5, 2025, litakapotajwa tena.

Related Posts