Unguja. Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), imeanzisha Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki (ISQMT) utakaondoa urasimu katika huduma hizo.
Akizindua mfumo huo leo Alhamisi Februari 20, 2025, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema wananchi wengi walikuwa wanapata usumbufu unaotokana na urasimu usio wa lazima wanapofuata huduma.
Amesema hali hiyo imechangiwa kwa kukosekana kwa mifumo ya kidijitali ya utoaji huduma ambayo sio tu hurahisisha utoaji huduma badala yake ingeepusha makutano ya mtu kwa mtu na kuweka uwazi katika utoaji huduma hizo.
“Mfumo huu unaozinduliwa leo umezingatia kuondoa changamoto na usumbufu uliokuwepo kwa muda mrefu ikiwamo upatikanaji wa huduma kwa uwazi, ufanisi na kwa wakati,” amesema Abdulla.
Pia, Abdulla ameziagiza taasisi zote za Serikali kuanzisha mifumo ya kielektroniki itakayowarahisishia wananchi kupata huduma kwa haraka na ubora.
Pia, amesema ni vyema kila mmoja akafahamu ubora wa bidhaa ni suala linalogusa maisha ya wananchi, hivyo wanapozungumzia maendeleo ya viwanda hawawezi kupuuza umuhimu wa viwango na mifumo madhubuti ya usimamizi wa ubora wa bidhaa.
“Ni wazi kuwa mfumo wa ISQMT utaleta faida ikiwamo kurahisisha mchakato wa kuthibitisha ubora wa bidhaa, kuhakikisha uwazi katika udhibiti, kurahisisha huduma kwa wazalishaji kwa wafanyabiashara na watumiaji,” amesema Abdulla.
Sambamba na hilo amesema, mfumo wa ISQMT utaiwezesha taasisi ya viwango kuwa na uwezo wa kufuatilia bidhaa kwa usahihi, kutoa vyeti vya ubora kwa haraka na kuwezesha wadau wote kupata taarifa kwa njia ya kidijitali.
Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango vya kimataifa.
Mfumo huo utasaidia wazalishaji wa ndani kuzingatia ubora, kuongeza imani kwa walaji na kuziwezesha bidhaa kupenya katika masoko mapya.
Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Yussuph Majid Nassor amesema mfumo huo hadi kukamilika kwake umegharimu Dola 400,000 za Marekani (sawa na Sh1.45milioni).
Amesema, mfumo huo umeamza miaka miwili iliyopita ambao umejumuisha wadau wote wa taasisi hiyo, wakiwamo mawakala, wajasiriamali na wafanyabiashara.
“Hiki kilikuwa kilio cha Serikali kwa muda mrefu kwa taasisi hii kuanzisha mfumo utakaowarahisishia wananchi kupata bidhaa zenye ubora na zitakazoingia katika masoko ya kikanda,” amesema Yussuph.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa taasisi hiyo, Monica Hangi amesema wamejiandaa kuboresha mazingira ya wafanyabiashara na kutoa vyeti vyenye ubora kwa kipindi kifupi.
Amesema mfumo huo utaonesha uwazi wa mchakato wa biashara na kuongeza mapato ya Serikali.
Pia, amesema kupitia mfumo huo utaongeza viwango vya kufikia soko la biashara katika bidhaa zinazofanyiwa uhakiki katika taasisi hiyo.
Mkurugenzi wa Mamlaka Serikali Mtandao (EGAZ), Seif Said Seif amesema wakati dunia ikielekea kuwa ya kidijitali taasisi zote zinalipwa kurahisisha utaratibu ili kupunguza gharama.
Hivyo, amezitaka taasisi za Serikali kuwa tayari katika mabadiliko ya kidijitali na kuzingatia miongozo kutoka mamlaka hiyo.
“Mfumo huu utarahisisha na kuongeza imani kwa wananchi na wafanyabiashara juu ya upimaji wa viwango vya biashara ili kupata bidhaa zenye viwango,” amesema Seif.