Mradi wa kuboresha ulinzi wazinduliwa mikoa ya kusini

Lindi. Wananchi wa mikoa ya Kusini wametakiwa kuacha tabia ya kumaliza kesi za ukatili nyumbani na badala yake watoe taarifa kwenye vyombo husika ili kuweza kuondoa changamoto hizo.

Wito huo umetolewa leo Alhamisi Februari 20, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva wakati wa  uzinduzi wa mradi wa kuboresha ulinzi kwa mikoa ya kusini kwa kushirikisha Jeshi la Polisi na wanajamii uliofanyika Manispaa ya Lindi mkoani Lindi.

Mkuu huyo wa wilaya amebainisha kuwa kuna baadhi ya wananchi humaliza kimya kimya kesi zinazohusu matukio ya ukatili wakikwepa kutoa taarifa kwenye vyombo husika.

“Wananchi wengi wamekuwa wakimaliza kesi za ukatili kimya kimya majumbani bila kutoa taarifa na kufanya matukio hayo kuendelea kuwepo.

“Ninaamini kuwa mradi huu utaweza kumaliza changamoto zote za wananchi kwa kuto kumaliza kesi kienyeji,” amesema Victoria.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Global Peace Foundation Tanzania (GPF), Hussein Sengu amesema kuwa malengo makubwa ya mradi huo ni kuboresha masuala ya Ulinzi na Usalama kwa kushirikisha polisi jamii na wanajamii wakiwemo wanawake na vijana.

Sengu amesema kuwa wanashirikiana na wadau mbalimbali chini ya udhamini wa ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania, ambapo mradi huo utatekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Amesema mradi huo pia unatarajiwa  kuboresha ushirikiano baina ya vyombo vya ulinzi katika mikoa ya Ruvuma, Lindi na hasa katika wilaya za Nyasa na Nachingwea,

“Malengo yetu ni kuhakikisha tunaweka mifumo bora ya kiutendaji katika kushirikisha wanawake kwenye ulinzi shirikishi,” amesema Sengu.

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mohamed Moyo amesema utekelezaji wa mradi huo utasaidia kupunguza uhalifu kwenye maeneo yao.

“Mradi huu unakwenda kupunguza changamoto za uhalifu katika maeneo yetu hasa kwenye maeneo ambayo yamekuwa na muingiliano wa watu katika nchi za jirani kama vile msumbiji na Malawi.”amesema Moyo.

Naye, Naibu Kamishna wa jeshi la polisi na mkuu wa dawati la ushirikishwaji kamisheni ya polisi jamii kutoka makao makuu ya jeshi Dodoma, Henry Mwaibambe amesema wamepokea mradi huo ikiwa ni mwendelezo wa miradi waliyonayo kwani mradi huo unakwenda kufanya kazi kwenye kata ambazo tayari askari wao wapo.

Pia, amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kuibua changamoto mbalimbali kwenye jamii.

“Niwatake wananchi kushirikiana na jeshi la polisi katika kuibua changamoyo za kwenye jamii kwani kuna matukio mengi ya kihalifu kwenye maeneo yetu hatuyatolei taarifa,” amesema Mwaibambe.

Sauda Mbung’o mkazi wa Mtange Manispaa ya Lindi, amelishukuru Shirika hilo kwa kuweza kusaidia jamii na kushirikisha wanawake katika kulinda amani kwa kujiunga na ulinzi shirikishi. “Kwa mpango huo tutaweza kuondoa uhalifu kwenye maeneo yetu kwani sisi wanawake tumekuwa hatupewi nafasi na kuonekana hatuwezi,” amesema Mbung’o.

Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa awamu mbili ikianzia na kutambua mahitaji, kushirikisha jamii, kutengeneza mtaala wa mafunzo, kufanya majaribio ya mtaala wa mafunzo, kufanya kampeni za kuongeza ulewa wa jamii juu ya ulinzi shirikishi na kusaidia juhudi za pamoja za wanawake.

Related Posts