Ridhiwani akemea ucheleweshaji fidia WCF, ahoji safari za watendaji nje ya nchi

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete amekemea safari za mara kwa mara za baadhi ya watenda Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) huku akihoji safari za kila mara za watendaji nje ya nchi.

akitaka zipunguzwe na tathmini ifanyike kabla mtu hajasafiri.

Pia ameutaka mfuko huo kuhakikisha unasimamia haki katika ulipaji wa fidia na kwa wakati kwa watu walioumia kazini kwa kuwa jambo hilo linawaumiza Watanzania.

Ametoa maagizo hayo leo Alhamisi Februari 20, 2025 alipozungumza na wafanyakazi wa WCF, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuteuliwa kushika nafasi hiyo ya uongozi.

Ridhiwani amesema safari zinazofanywa na baadhi ya watu ndani ya WCF hazina tija na hivyo amemtaka mkurugenzi kufanya tathmini ya kila pendekezo la safari linalokuja, ili kujua faida ya mtu huyo kusafiri.

“Ukikaa ukiangalia, mara yuko Ujerumani, Marekani, Afrika Kusini unabaki unajiuliza na wanaosafiri ni watu walewale. Nikuombe sana mkurugenzi, mtu anapotaka kusafiri atwambie faida tutakayoipata kwa safari yake na tuzione akirudi, sio kusafiri safari tu,” amesema Ridhiwani.

Akitolea mfano wa bajeti aliyopelekewa mezani kwake, amesema inaonyesha matumizi ya shirika ni makubwa kuliko makusanyo hivyo amtaka katibu mkuu wa wizara hiyo akae na timu wataalamu waone watakavyoipunguza.

“Niwaambie tu hakutakuwa na huruma katika hili, kama mtatuchukia tuchukieni lakini hatuwezi kuruhusu safari nyingi faida inayopatikana hakuna.

“WCF safari ni nyingi, sawa mnazo kazi za kwenda kufanya sikatai, lakini nikisema watu ambao wamesafiri waniletee taarifa zao tutaingia katika mgogoro mkubwa, sifa ya Serikali si kusafiri ni kuhudumia kwa kutoa fidia kwa wanaotakiwa na kulipa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Ridhiwani amewataka WCF kuangalia namna ya kufanya uwekezaji kwa kile alichoeleza kuwa sheria inawaruhusu kuwekeza fedha za wanachama ziweze kuzaa na kuleta tija katika mfuko.

“Ziko aina za uwekezaji ambazo ni salama na zina faida na zipo ambazo si salama. Uwekezaji salama upo, uwekezaji unaokupa nafasi ya kupata fedha nyingi,” amesema Ridhiwani.

Amewataka wakuu wa vitengo mbalimbali kukaa na kufikiria ni sehemu gani wanazoweza kuwekeza, hasa kwa kujifunza katika maeneo ambayo wanasafiri.

“Huko mnakokwenda mkajifunze wenzenu wanavyofanya, siyo mnasafiri mkirudi huku hakuna mabadiliko yoyote mnatuletea risiti za marejesho, hatutaki retirement (marejesho), tunataka tuone mabadiliko ya uwekezaji, hayo ndiyo maeneo ya msisitizo,” amesema.

Pia amewataka kuangalia vizuri sera yao ya uwekezaji ili ilete tija na kuwapa uhakika pindi watakapowekeza ili wanachama waweze kunufaishwa na kilichofanyika.

Ridhiwani amewataka WCF kuhakikisha watu wanapata fidia zao ndani ya wakati na kuacha kuwapa sababu mbalimbali.

Alitolea mfano wa mtu aliyemtaja kwa jina moja la Mayala kutoka mkoani Geita ambaye alipata matatizo ya mgongo wakati akifanya kazi mgodini, lakini amekuwa akihangaika kupata fidia hadi malalamiko yake kufika ofisini kwake.

“Waoneeni huruma Watanzania, watu wameteguka viuno na migongo, humu ndani mnaandika huyu mtu hastahili kulipwa kwa sababu hili jeraha halijasababishwa na kazi, nyie mnataka ule mgodi umwangukie ndiyo useme ulemavu umesababishwa na kazi, kuweni na huruma nyie watu, hili shirika tunapita tu, leo uko hapa kesho upo kwingine,” amesema.

Amesema ni vyema kutosubiri ndugu wa mfanyakazi aumie ndiyo mtu ajue uchungu unavyokuwa pindi asipolipwa fidia na kuwa raha ya Serikali ni kuona shirika likilipa fidia kwa watu badala ya kujisifia kuwa na mabilioni ya shilingi yaliyobakia.

“Raha yake ni kuona shirika lifanye kazi iliyokusudiwa ya kulipa fidia, wasaidieni Watanzania. Watanzania wanaumia, wanaumia kwelikweli, lakini ninyi kwa upande wenu mnaona kama ni mzaha mzaha,” amesema Ridhiwani.

Amewataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa haki na moyo ili kuondoa laana inayoweza kulikumba shirika hilo.

Katika hatua nyingine, Ridhiwani ameitaka WCF kuongeza nguvu katika kusajili waajiri na kuhakikisha wanawasilisha michango ya watumishi wao kwa wakati ili kuwezesha watumishi hao kupata haki yao kwa wakati endapo watapata ajali, kuumia, ugonjwa au kifo kutokana na kazi zao vitawafikia.

“Natambua kuwa hadi sasa WCF imesajili asilimia 93.7 ya waajiri wote nchini, lakini hiyo haitoshi na ninaitaka menejimenti ihakikishe kwamba waajiri wote wanasajiliwa hadi kufikia asilimia 100 na wanawasilisha michango yao kwa wakati,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk John Mduma amesema menejimenti imepokea maelekezo ya waziri na kwamba watumishi wataongeza kasi ya uwajibikaji ili kutekeleza maagizo hayo.

“Tumepokea maelekezo ya Waziri ambaye ametutaka kuongeza kasi katika usajili wa waajiri na ukusanyaji wa michango, ulipaji wa mafao, tumelipokea na tutalifanyia kazi,’’ amesema Dk Mduma.

Akitoa salamu za shukrani mwakilishi wa wafanyakazi wa WCF, Musa Mwambujule amemshukuru Waziri kwa kuwatembelea na kuwasikiliza wafanyakazi, jambo ambalo limeonyesha namna ambavyo inawathamini.

Related Posts