Samia azindua tume za masuala ya Ngorongoro, uhamaji wa hiari

Dar es Salaam. Rais wa Samia Suluhu Hassan amezindua Tume ya Rais ya Kutathmini kuhusu masuala ya mgogoro wa ardhi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Tume ya Rais ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa wakazi wa eneo la hifadhi hiyo ikiwa ni siku 58 tangu kuteuliwa kwao.

Tume hii inazinduliwa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Desemba mosi, 2024 alipokutana na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai wanaoishi eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kutangaza uamuzi wa Serikali kuunda tume.

Taarifa ya kuzinduliwa kwa tume hizi imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Sharifa Nyanga leo Februari 20, 2025. Uzinduzi wa Tume hizo mbili umefanyika Ikulu Magogoni jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Samia amesema anaamini kuwa kazi itakayofanywa na tume hizo itawezesha kupatikana kwa suluhu ya kudumu.

“Ninaamini kuwa kazi itakayofanywa na Tume hizi itawezesha kupatikana kwa suluhu ya kudumu ya changamoto zilizowasilishwa kwangu na viongozi na wawakilishi wa wananchi wanaoishi kwenye eneo la Ngorongoro,” amesema Samia.

Tume hizo mbili zitaongozwa na Jaji Dk Gerald Ndika ambaye ni Mwenyekiti wa tume ya kutathmini kuhusu masuala ya mgogoro wa ardhi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Mhandisi Musa lyombe ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya kutathmini zoezi la uhamaji wa hiari wa wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Tume hizo mbili zinajumuisha uwakilishi wa wananchi wanaoishi katika eneo la Ngorongoro na zinatarajia kufanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu.

Katika taarifa ya Desemba 24 mwaka jana, Dk Ndika atasaidiana na wajumbe tisa walioteuliwa katika timu yake akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Philemon Luhanjo.

Wengine ni Zakia Meghji, aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Jaji George Masaju ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu na Mshauri wa Rais, Sheria.

Pia, Dk Richard Muyungi ambaye ni Mshauri wa Rais, Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi ameteuliwa pamoja na Balozi Salome Sijaona ambaye ni Balozi na Katibu Mkuu mstaafu.

“Pia Rais amemteua, Profesa Wilbard Kombe ambaye ni Profesa wa Chuo Kikuu Ardhi, Profesa Emmanuel Luoga kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Mollel James Moringe Diwani na Katibu wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro na Moi Aprakwa Sikorei na Diwani na Mkazi wa Ngorongoro,” amesema.

Katika timu ya Musa Iyombe ambaye ni Katibu Mkuu mstaafu kuwa mwenyekiti wa tume hiyo atasaidiwa na wajumbe wanane, akiwemo Sihaba Nkinga ambaye ni Katibu Mkuu mstaafu.

Wengine ni Alphayo Kidata ambaye ni wa Rais, Uwezeshaji Biashara na Masuala ya Kodi, Balozi Valentino Mlowola na Balozi Mstaafu na aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Wengine Balozi mstaafu na aliwahi kuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Balozi Mohamed Mtonga, Balozi mstaafu, Balozi George Madafa, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (NHC), Haruna Masebu.

“Wengine walioteuliwa Edward Maura Nduleti na Rehema Moisare ambaye ni Mwalimu na Mkazi wa Ngorongoro,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Related Posts