Serikali yazindua “Sitapeliki” kudhibiti vitendo vya utapeli, ulaghai mitandaoni

Arusha. Serikali imeanzisha kampeni maalumu kwa ajili ya kudhibiti vitendo vya utapeli na ulaghai mitandaoni ambavyo husabanisha hasara kwa watu binafsi na Taifa kwa ujumla na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Kampeni hiyo imezinduliwa leo Alhamisi Februari 20, 2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, wakati wa kikao kazi kati ya Serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano, kilichofanyika jijini Arusha.

Slaa amesema kampeni hiyo ijulikanayo kama ‘Sitapeliki’, imelenga kutoa elimu kwa umma na kuwa na mpango mahsusi wa kushughulikia masuala ya utapeli na ulaghai mitandaoni.

Pia, itatumika kuongeza uelewa kuhusu mbinu zinazotumiwa na matapeli wa mtandaoni na kuwapa taarifa zaidi ya jinsi ya kujikinga na majaribio mbalimbali ya ulaghai na kujiepusha na udanganyifu, unaofanywa na watu wachache wenye lengo la kujinufaisha binafsi.

“Kampeni hii ya ‘sitapeliki’ inalenga kutoa elimu kwa jamii kuchukua hatua mahsusi na jumbe mbalimbali zitasambazwa ili kukumbusha jamii kuhusu kuchukua tahadhari na kuepukana na utapeli mtandaoni,”

Waziri Slaa amesema ulaghai na utapeli unaleta hali ya watumiaji kuogopa kufanya miamala yakidijiti, jambo linaloathiri juhudi za Serikali kueneza huduma mbalimbali za jamii na za kiuchumi kupitia mitandao.

 “Utapeli unahujumu mikakati ya Serikali kuendeleza ushirikishwaji wa wananchi kwenye mifumo ya kifedha na kujenga uchumi wa kidijiti. Ni matumaini yangu kwamba baada ya kuzindua kampeni hii kila mdau ataenda kutekeleza kwa wakati mpango huu mahususi, ambao utafanikisha lengo la kupeleka elimu na uelewa katika jamii juu ya kujikinga dhidi ya vitendo hivi,” amesema.

“Usalama na uimara wa mitandao unaongeza imani ya wananchi kutumia mifumo ya Tehama, jambo ambalo linachochea ushiriki wao kikamilifu katika uchumi wa kidijiti. Natambua mchango mkubwa wa watoa huduma kutoka katika kampuni za simu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,” ameongeza.

 Awali akizungumzia kikao kazi hicho Waziri huyo ametaja mafanikio yaliyofikiwa katika sekta hiyo ni pamoja na ufikishwaji wa mawasiliano ya mkongo wa taifa katika wilaya 109 hati ya 139 nchini, sawa na asilimia 78.

Amesema hadi kufikia Desemba 2024 kadi za simu za mkononi zilizosajiliwa ni milioni 86.8 hivyo kuwezesha Serikali kukusanya mapato kutokana na huduma za kidijitali.

Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Khamis Abdulla amesema kikao kazi hicho kimelenga kutathmini utekelezaji wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa miaka 10 kuanzia 2024 hadi 2034.

Amesema mkakati huo utakuwa na nguzo sita ambazo ni kuwezesha miundombinu ya kidigitali, utawala na mazingira wezeshi, uelewa wa kidigitali na maendeleo ya ujuzi, utamaduni wa ubunifu wa kidigitali na teknolojia wezeshi.

Nyingine ni kukuza ushirikishwaji wa kidigitali na ufikivu na huduma za kifedha za kidigitali.

Mmoja wa wakazi wa Kata ya Sekei,jijini Arusha, Juliana Assey, amesema kampeni ya Sitapeliki itasaidia kupunguza vitendo vya kihalifu mitandaoni.

Related Posts