Droo ya robo fainali ya Kombe la Shrikisho Afrika imepangwa ambapo Simba itavaana na Al Masry ya Misri.
Simba ambayo ndiyo timu pekee ya Tanzania iliyobaki kwenye mashindano ya Caf baada ya Yanga, Coastal Union na Azam kuondolewa itaanzia ugenini ambapo mchezo wa kwanza utapigwa Aprili 4 huku wa pili ukipigwa Aprili 10 kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.
Hii ni nafasi ya Simba kufuzu kwa mara ya kwanza kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kukwamia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara kadhaa na Kombe la Shirikisho.
Hii itakuwa mara ya pili kukutana na Al Masry ambapo mwaka 2018, timu hizo zilikutana raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho na Simba kuondolewa kwa faida ya bao la ugenini.
Katika mchezo ambao ulipigwa kwa Mkapa mechi ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2, mchezo ambao ulitawaliwa na mvua kubwa, lakini walipokwenda ugenini mechi ikaisha kwa suluhu na Simba kuondolewa.
Endapo Simba ikifuzu kwa hatua ya nusu fainali, basi inaweza kujikuta inarudi tena Misri kwa kuwa itavaana na mshindi wa mchezo kati ya Zamalek ya Misri au Stellenbosch ya Afrika Kusini kwenye hatua ya nusu.
Hii ina maana kama Simba ataingia fainali inaweza kukutana na Asec au RS Berkane au CS Constantine ambao wamepangwa kukutana na USMA kwenye robo fainali ya michuano hii.