Arusha. Serikali imesema ipo tayari kurudi kwenye meza ya mazungumzo na wadau wa sekta ya mawasiliano kutathmini utekelezaji wa sheria inayozitaka kampuni za simu kuuza asilimia 25 ya hisa zake kwa umma kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Kauli hiyo inakuja huku kukiwa na taarifa za kuwepo kwa Watanzania walionunua hisa kwenye Kampuni ya Simu ya Vodacom Tanzania mwaka 2017 kutofahamu hatima yao ikiwemo kupata gawio.
Awali, Vodacom Tanzania ilikuwa ya kwanza kutekeleza Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Epoca) na Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 kwa kujisajili na kuuza asilimia 25 ya hisa zake kwa umma kupitia DSE.
Wakati Vodacom inaingia kwenye soko la hisa, Serikali iliwataka Watanzania kujitokeza na kununua hisa hizo baada ya kusoma na kuuelewa waraka wa matarajio wa kampuni hiyo.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema hayo leo Alhamisi, Februari 20, 2025 kwenye kikao kazi cha watendaji wa wizara hiyo na wadau kujadili utekelezaji wa mkakati wa miaka 10 wa uchumi wa kidijitali (2024 hadi 2034).
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema kuwa Serikali ipo tayari kurudi kwenye meza ya mazungumzo na wadau wa sekta ya mawasiliano ili kutathmini utekelezaji wa sheria iliyotungwa mwaka 2017 iliyokuwa ikizitaka kampuni za simu kuuza asilimia 25 ya hisa zake kwa umma kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Amesema kuna changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa sheria hiyo licha ya hatua zilizochukuliwa na kampuni za simu ikiwemo Vodacom na kwamba, bado kuna masuala yanayohitaji marekebisho.
Silaa amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau, itafanya tathmini ya hatua zilizochukuliwa hadi sasa ili kuboresha utaratibu na kuhakikisha sekta ya mawasiliano inakua na tija na faida kwa pande zote.
“Napata maswali mengi lini wengine watajiunga, lakini vilevile kwa maelezo yako performance ya wale waliotangulia haijawa nzuri. Nadhani njia bora zaidi ya kukuza sekta yoyote kwenye uchumi huu wa soko ni kuacha sekta zitawaliwe na nguvu ya soko.
“We as Government (sisi kama Serikali) tukianza kutengeneza shuruti kwenye baadhi ya mambo matokeo yake ndiyo haya, unachosema sina tathmini sahihi lakini, ndiyo hicho ulichokisema.
“Lakini, ninachoweza kusema nadhani ni wakati sahihi sisi kama Serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwa sababu tuna wadau, tutakaa tuangalie tulipotoka, maamuzi tuliyoyafanya, tulipo ili tutengeneze utaratibu mzuri huko tunapokwenda,” amesema Silaa wakati akijibu moja ya maswali yaliyoulizwa na wadau kwenye kikao hicho.
Amesema ni wakati muafaka kwa Serikali na wadau kukaa ili kutengeneza njia bora zaidi ya kampuni hizo kujiendesha kwa kuweka miongozo yenye kukidhi matarajio ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Sheria tunazitunga ili kurahisisha mambo kwa utaratibu sio kutufunga kwa kuwa sheria sio msaafu. Wabunge wapo hapa, Kamati ya Bunge ipo. Nadhani ni wakati muafaka wa sisi kukaa na kutengeneza njia bora zaidi kwa kampuni hizi kujiendesha, hasa tukiweka mazingatio kwenye miongozo na matarajio aliyonayo Rais Samia. Rais wetu amefanya kazi kubwa kwenye kutengeneza, kukuza mazingira ya uwekezaji nchini,” amesema Silaa.