Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeonya uwepo wa hali mbaya ya hewa kwa siku tano katika mikoa mitano nchini pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Hali mbaya inayoelezwa kuathiri mikoa mitano ni upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi yanayofikia mita mbili.
Mikoa itayoathirika kuanzia kesho Ijumaa Februari 21, 2025 ni maeneo ya ukanda wa Pwani ya kaskazini ya bahari ya Hindi yenye mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani na visiwa vya Mafia, Pemba na Unguja.
Taarifa hiyo ya TMA imetolewa leo Alhamisi Februari 20, 2025 ikieleza hali mbaya ya hewa itashuhudiwa kuanzia Februari 21 na 22, 2025 lakini Februari 20, 23 na 24 hakuna tahadhari iliyotolewa.
Februari 22, 2025 mikoa inayopaswa kujiandaa ni upepo mkali ni Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara, visiwa vya Mafia na visiwa vya Unguja na Pemba.
“Kiwango cha athari zinazoweza kutokea ni wastani, athari zinazoweza kujitokeza ni kuathirika kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi, uvuvi na usafirishaji baharini,” imeandikwa kwenye taarifa hiyo ya TMA.