Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo, kinatarajiwa kukaa katika vikao vyake vya ngazi ya juu kutathmini kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa na mwelekeo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Vikao hivyo ni Halmashauri Kuu itakayofanyika Februari 23, ikitanguliwa na Kamati Kuu itakayoketi Februari 22, mwaka huu katika Ukumbi wa Maalim Seif, Dar es Salaam.
Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, tayari chama hicho kimeshafungua pazia la wanachama wake kutia nia katika nafasi mbalimbali ikiwemo ya urais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.
Kwa upande wa Jamhuri ya Muungano, Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu ameshatangaza nia, huku Masoud Othman akitangaza nia kwa upande wa Zanzibar.
Hata hivyo, vikao hivyo viwili pamoja na mambo mengine, vinatarajiwa kukamilisha ratiba ya chama hicho kuelekea uchaguzi kama ilivyowahi kuelezwa na Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu alipozungumza na gazeti hili.
Taarifa ya kufanyika kwa vikao hivyo, imetolewa leo, Ijumaa Februari 21, 2025 na Naibu Katibu Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, halmashauri kuu itapokea taarifa ya kina ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 na wajumbe watafanya tathmini na kukiagiza chama hicho hatua muafaka za kuchukua.
“Halmashauri kuu pia, itajadili na kutoa mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi mkuu,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa chama hicho, halmashauri kuu ni kikao cha pili kwa ukubwa baada ya Mkutano Mkuu.
Mbali na wajumbe wa kuchaguliwa, halmashauri kuu inaundwa na wenyeviti na makatibu wa mikoa yote ya kichama, Bara na Zanzibar.