UNAIKUMBUKA ile mechi ya kwanza kwa kocha mpya wa Yanga, Hamdi Miloud alipovaana na JKT Tanzania na kulazimisha suluhu kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo?
Katika mechi ile kuna mabeki wawili walichezea sifa kwa kuwazuia kabisa nyota wa Yanga, akiwamo Clement Mzize, Prince Dube na Stephane Aziz KI kuendeleza moto wa kugawa dozi kwa wapinzani.
Sasa mmoja wa mabeki hao, Wilson Nangu aliyechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa pambano hilo, ameingia kwenye anga za vigogo hao wakidaiwa kumpiga hesabu ili kumng’oa jeshini.
Inadaiwa, beki huyo aliyesimama imara sambamba na Edson Katanga mbele ya mastaa wa Yanga na kulazimisha mechi kuisha kwa suluhu kwa msimu wa pili mfululizo kwenye uwanja huo anahitajiwa na Yanga kwa msimu ujao na tayari menejimenti yake imeshafuatwa ili kujua taratibu za kumng’oa.
Hata hivyo, inaelezwa dau ambalo mabosi wa mchezaji huyo wamewatajia Yanga, huenda wakaingiwa na ubaridi, ingawa lolote linaweza kutokea.

Inaelezwa, Yanga imetakiwa kuweka mezani Sh300 milioni ili kuvunja mkataba alionao JKT kama kweli inataka kumng’oa, mbali na makubaliano na mchezaji huyo aliyekuwa akiitumikia TMK Stars iliyopo Ligi ya Championship kabla ya kunyakuliwa timu aliyopo sasa.
Inaelezwa Yanga inasaka beki mwingine wa kati ili kusaidiana na nahodha Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job, na kiwangio kilichoonyeshwa na beki huyo wa JKT kimewavutia mabosi hao na kupisha hodi jeshini.
Chanzo cha ndani kutoka JKT Tanzania kinasema; “Ni kweli Yanga imekuja kuomba iuziwe beki huyo hivyo imepewa dau la kuvunja mkataba ambalo ni Sh300 milioni, kisha itaendelea na mazungumzo na mchezaji mwenyewe kukubaliana mambo ya mshahara na ishu nyingine za kimasilahi.”
Mbali na Nangu, mapema Yanga ilianza mazungumzo na beki wa Coastal Union, Lameck Lawi ambaye msimu huu alitambulishwa Simba kabla ya dili hilo kukwama baada ya Wagosi kurejesha fedha kwa kilichoelezwa Msimbazi walikiuka makubaliano ya mauzi ya mchezaji huyo. Yanga bado inampigia hesabu beki huyo wa kimataifa wa Tanzania.
Ukiachana na hao, Yanga pia inaelezwa kama dili la Nangu na Lawi yatakwama kwa ajili ya kuimarisha safu yao ya ulinzi, ina mpango wa kumtumia aliyekuwa beki wa kati wa timu ya vijana ya Yanga anayekipiga kwa sasa Wakiso Giants ya Uganda, Shaibu Mtita.

Mtita anayecheza kwa mkopo Wakiso baada ya kupandishwa kutoka kikosi B na aliyekuwa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi na alicheza mechi chache za Kombe la Mapinduzi na lile la Shirikisho (FA).
Rekodi zinaonyesha katika mechi 16 za Ligi Kuu Uganda, Mtita kacheza mechi 14 kwa dakika 1031 akiruhusu mabao 23, huku mechi yake ya kwanza ilikuwa Septemba 15 dhidi ya Bright Stars ilikuwa sare ya 1-1 alimaliza dakika 90.
Mechi nyingine ni dhidi ya Maroons 2-3 akimaliza dakika 90, Mbale Heroes 0-1 (83), UPDF 1-0 (90), Vipers 2-0 (90), Express 0-0 (15), Lugazi 0-0 (7), Villa 6-1 (26), URA SC 3-0 (90), Police 2-1 (90), Mbarara City 0-0 (90), Kitara 0-0 (90), BUL 1-1 na Villa 1-1 akimaliza dakika (90).