Babati. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Ally Hapi amewataka viongozi wa vyama vya upinzani kutolalamika kwa watu na kutoa visingizio kuwa wanataka Katiba mpya na Tume mpya ya uchaguzi ili hali watu hawawezi kula hayo wanahitaji maendeleo.
Hapi amewataka viongozi wa vyama vya upinzani kutoogopa kushiriki uchaguzi, akisisitiza kuwa kazi kubwa zilizotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan zinatosha kukipa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ushindi wa kishindo.
Akizungumza mjini Babati leo Ijumaa Februari 21, 2025, Hapi amesema kinachohitajika kwa jamii ni miradi ya maendeleo ya maji, afya, elimu na miundombjnu na siyo kula ugali wa katiba au kukoroga uji wa Tume mpya ya uchaguzi.
“Maendeleo haya ya miradi mikubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni dhahiri kuwa yanaonekana na hayahitaji propaganda za kisiasa, hivyo wapinzani wajipange,” amesema Hapi.
Amesema kipindi cha uongozi wa awamu ya nne ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, mwaka 2014, viongozi wa vyama vya upinzani waligomea mchakato huo na kuibuka mwaka 2025 kudai hayo.
“Waache visingizio vya kutaka katiba mpya na tume mpya, washiriki uchaguzi kwani CCM imefanya kazi kubwa, tumeshuhudia miradi mingi ya maendeleo, kuboreshwa kwa huduma za kijamii na uimarishaji wa uchumi,” amesema Hapi.
Amesema kuwa CCM itaendelea kuaminika kwa Watanzania kutokana na utekelezaji wa ilani yake kwa vitendo huku akiwataka wanachama wa chama hicho kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu mafanikio hayo.
Kauli ya Hapi inakuja wakati vyama vya upinzani vikiendelea kueleza changamoto mbalimbali zinazokumba mazingira ya kisiasa nchini huku baadhi yao wakidai kuwa bila Tume mpya ya uchaguzi hakuna uchaguzi.
Chadema, kupitia kaulimbiu yake ya “NoReforms, No Election” (Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi), kimekuwa kikisisitiza kwamba kinakwenda kushinikiza mabadiliko ya msingi kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, hasa kupata Tume Huru ya Uchaguzi.

Hata hivyo, Hapi amevitaka vyama vya upinzani kutokimbia uchaguzi kwani CCM ina uhakika wa kushinda kutokana na kazi zilizofanyika kupitia serikali ya awamu ya sita.
Akiwa mjini Babati ametembelea shina namba moja la CCM, Mtaa wa Old Majengo ambako alizungumza na wanachama na kusikiliza kero.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Manyara, Janes Darabe amesema maendeleo yaliyofanyika kupitia serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkoa huo ni zaidi ya Sh700 bilioni.
“Sisi hatuna cha kumlipa Rais Samia lakini tunamshukuru na tunasubiri Oktoba 2025, tunampa kura nyingi za kutosha na kuongoza nchini kwa kumpa kura nyingi za ndiyo,” amesema Darabe.
Mwenyekiti wa Wazazi Wilaya ya Babati Mjini, Emmanuel Khambay amesema wanapata ushirikiano mkubwa kupitia viongozi wa CCM na Serikali kwa ujumla katika uongozi wao.
“Mambo yote ya kikanuni yanafanyika kwa ushirikiano mkubwa na wakutosha katika kuhakikisha tunatekeleza wajibu wetu ipasavyo,” amesema Khambay.
Mmoja kati ya madereva wa pikipiki za kubebea abiria (bodaboda), Mrisho Juma amesema wamepatiwa mikopo kupitia halmashauri ya mji, hivyo wanaishukuru Serikali.