Watu wenye kisukari ambao hawajaweza kuthibiti viwango vya sukari, wapo kwenye hatari kubwa ya kupata matatizo katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, ikiwa ni pamoja na tumbo kujaa gesi na vidonda vya tumbo.
Matatizo haya yanaweza kusababisha usumbufu mkubwa kwa wenye kisukari, hasa upande wa lishe sahihi na matibabu.
Watu wenye kisukari mara nyingi hukumbwa na matatizo ya gesi kutokana na mabadiliko ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na aina ya chakula wanavyokula, lakini pia kutoweza kuthibiti viwango vyao vya sukari.
Viwango vya juu vya sukari vinaweza kuathiri umeng’enyaji wa chakula na kusababisha gesi tumboni na vidonda vya tumbo.
Vidonda vya tumbo ni hali inayosababishwa na uharibifu wa ukuta wa tumbo au sehemu ya juu ya utumbo mdogo.
Kwa watu wenye kisukari, vidonda vya tumbo na tumbo kujaa gesi vinaweza kuwa sugu na kupona polepole kutokana na ukubwa wa tatizo na sababu kuu za vidonda vya tumbo ni maambukizi ya bakteria.
Dalili za vidonda vya tumbo na tumbo kujaa gesi kwa wenye kisukari ni pamoja na kupata maumivu makali ya tumbo, hasa wakati wa kula au baada ya kula, kichefuchefu na kutapika.
Nyingine ni upungufu wa damu unaosababisha uchovu na udhaifu, kula chakula kidogo na kushiba haraka.
Lishe bora ni silaha muhimu kwa wagonjwa wa kisukari wanaopata matatizo ya gesi na vidonda vya tumbo. Baadhi ya vyakula vinavyopendekezwa ni vyakula vinavyosaidia mmeng’enyo wa chakula kama mboga za majani zikiwamo mchicha, sukuma wiki, na kabichi laini, matunda yenye nyuzinyuzi kama mapapai, ndizi mbivu, tikiti maji na tufaha.
Pia kuna nafaka zisizokobolewa kama ulezi, mtama, uwele, shayiri, ngano na viazi vilivyochemshwa au kuchomwa bila viungo vingi.
Wanashauriwa pia kula protini isiyo na mafuta mengi kama maharagwe laini, samaki na kuku. Ila wasitumie ngozi ya kuku kwani ina mafuta mengi.
Aidha, wanaweza kutumia tangawizi, mdalasini kwenye maji ya uvuguvugu au chai kusaidia kupunguza gesi.
Vyakula vyenye mafuta mengi na kukaangwa kama chipsi na nyama ya kukaanga havifai.
Vingine ni vyakula vyenye sukari nyingi kama soda, juisi za viwandani, na vile vilivyosindikwa.Pia waepuke vinywaji vyenye gesi na kafeini kama kahawa na soda na vile vyenye viungo vingi na vikali kama pilipili.
Kwa wagonjwa wa kisukari, matatizo ya gesi na vidonda vya tumbo yanaweza kuwa changamoto kubwa, lakini yanaweza kudhibitiwa kwa mbinu sahihi za lishe na matibabu.
Kufuatilia kiwango cha sukari, kula chakula chenye virutubisho sahihi, na kuepuka vyakula vinavyochochea matatizo ya tumbo ni hatua muhimu.
Ni vyema pia wakashauriana na daktari au mtaalamu wa lishe kwa mwongozo sahihi wa kiafya.