Huyu Camara ana balaa | Mwanaspoti

KIPA wa Simba, Moussa Camara ‘Spider’ ameendelea kuthibitisha thamani yake tangu aliposajiliwa na Wekundu wa Msimbazi hao, huku akiwapa furaha mashabiki wa klabu hiyo.

Camara alitua msimu huu akitokea AC Horoya ya Guinea, juzi alishuka uwanjani katika mechi ya 19 akiisaidia Simba kupata ushindi wa mabao 3-0, lakini akiandika historia kwa klabu hiyo katika Ligi Kuu Bara.

Kipa huyo amefikisha ‘clean sheet’ 15 akiifikia rekodi iliyowekwa msimu uliopita na aliyekuwa kipa wa Coastal Union, Ley Matampi, huku akionekana kuwa bora Ligi Kuu Bara, lakini ni kama amewazuga wenzake kwa kusema anachokifanya wala hashindani na yeyote.

Camara aliyesajiliwa msimu huu kutoka AC Horoya ya Guinea amesema licha ya kutoshindana na mtu, lakini hakomai sana uwanjani kwa lengo la kutafuta tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu wa msimu, isipokuwa kutimiza wajibu wake na kuhakikisha Simba inapata kile kilichowafanya wamsajili.

Clean sheet alizonazo Camara, zimemfanya amuache kwa mbali kipa wa Yanga Diarra Djigui mwenye tisa, lakini akiwazidi tano makipa Patrick Munthali wa Mashujaa na Mohammed Mustafa (Azam) wenye 10 kila mmoja hadi sasa.

Hata hivyo, kipa huyo alisema clean sheet anazofanya hazina maana anashindana na mtu ama kuisaka Tuzo ya Kipa Bora wa msimu isipokuwa kuhakikisha timu yake inafanya vizuri na kutimiza malengo aliyonayo na yale ya timu kwa msimu huu katika michuano yote.

Akiwa amecheza mechi 19 msimu huu na kudawa zote kwa dakika 1,710 huku timu hiyo ikifunga mabao 41 na kukusanya pointi 50, mbili pungufu na alizonazo Yanga iliyocheza mechi moja zaidi ikiwa na 20, wakati Simba imecheza 19 hadi sasa.

Msimu uliopita Matampi alimaliza na ‘clean sheet’ 15 kwa msimu mzima akicheza mechi 24 kati ya 30 za ligi ikiwa ni sawa na dakika 2,160, kitu kinachomfanya Camara kuwa katika nafasi nzuri ya kuipita rekodi hiyo na kuiweka yake kwani timu anayocheza imeswaliwa na michezo 11 kwa sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Camara alisema japo anafanya vizuri ila haangalii hesabu za kuwa amefikisha ‘clean sheet’ ngapi katika ligi hiyo kwani sio kipaumbele chake.

Alisema kitu muhimu anachoangalia ni namna timu yake inatoka salama kwa ushindi ili wafikie malengo yao msimu huu.

“Sitaki kuweka akili ya kuanza kujipambanisha na makipa wengine kwa kuwa ligi bado mbichi, huku presha ni kubwa kwenye kuwania ubingwa msimu huu.

“Kitu cha muhimu zaidi ni kutimiza wajibu wangu wa kuhakikisha timu yangu hairuhusu mabao, ili mwisho tumalize kwa kutimiza malengo yetu ya msimu.”

Related Posts