Kamati ya PAC yaibua kasoro utendaji taasisi za Serikali

Unguja. Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) ya Baraza la Wawakilishi, imesema katika utendaji kazi wake imebaini kasoro nyingi, ikiwemo taasisi za Serikali kutofanya usuluhishi wa kibenki, hivyo kusababisha kuwepo tofauti baina ya taarifa za fedha za benki na zile za fedha taslimu za taasisi.

Kutokana na hilo PAC imesema kumekuwa kukiibuka hoja kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kamati imebaini kuwa changamoto hiyo husababishwa na uhifadhi mbaya wa kumbukumbu za mapato na matumizi ya fedha za Serikali, hivyo kusababisha kuwepo tofauti ya taarifa za kifedha maeneo hayo mawili.

Hayo yamelezwa katika ripoti ya PAC iliyowashilishwa barazani na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Juma Ali Khatib leo Februari 21, 2025.

“Changamoto hii husababishwa na uwepo wa baadhi ya maofisa masuuli ambao hushindwa kuwasimamia ipasavyo watendaji wao, hususani maofisa uhasibu wa taasisi hizo,” amesema.

Amesema kamati imebaini wakati wakaguzi kutoka Ofisi ya CAG wanapofika kwenye wizara za Serikali au taasisi zake kutekeleza majukumu yao, hukumbana na mazingira magumu ya kutopatiwa ushirikiano wa kutosha ikiwa ni pamoja na kutopatiwa vielelezo vilivojitosheleza au maelezo sahihi yanayothibitisha uhalali wa mapato au matumizi yaliyotekelezwa na watendaji wa wizara.

Amesema kamati imekutana na uhalisia huo ilipochunguza hoja za Shirika la Mawasiliano (Zictia), Chuo cha Mafunzo, Kamisheni ya Utalii, Jeshi la Kujenga Uchumi, Shirika la Nyumba, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca) na Wakala wa Karakana ya Magari Zanzibar. 

“La kushangaza wakati mkaguzi anapofika katika taasisi za Serikali huelezwa vielelezo au majibu hayapo lakini ikifika Kamati ya PAC, vielelezo vingi vinakuwepo ambavyo vinatosheleza kuzuia hoja kuingizwa katika kitabu cha ripoti,” amesema.

Miongoni mwa vigezo vya msingi ambavyo CAG huvitumia katika utoaji wa hoja za kiukaguzi ni taasisi nyingi za Serikali hushindwa kufunga ipasavyo taarifa za hesabu za mwisho wa mwaka au hushindwa kuwasilisha kwa wakati taarifa hizo. 

Mwenyekiti huyo amesema kamati imepitia taarifa za hesabu za mwisho wa mwaka za taasisi za Serikali na kubaini kuna baadhi hufunga hesabu zake zikiwa na upungufu mwingi ambao husababisha kutokutoa taswira kamili na sahihi ya hesabu hizo, hususani kwa wale watakaopata fursa ya kuzisoma au kuzitumia.

Mjumbe wa kamati hiyo, Mwanaidi Kassim Mussa amesema ni muhimu kuzingatia sheria.

Ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango kuendelea kutoa elimu kwa taasisi hizo na maofisa masuhuli.

Related Posts