Kocha Yanga amshangaa Aziz KI, afunguka jambo zito

Imekuwa ni mazoea watu wanaoana huwa na siku 7 za kukaa fungate kwa ajili ya kusherehekea kutimiza ibada hiyo ya ndoa, lakini kwa nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki ni kama suala hilo halipo kutokana na kuwa katika msafara wa wachezaji wa Yanga walioenda mjini Kigoma.

Yanga inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, kukabiliana na Mashujaa na Aziz KI ni mmoja ya wachezaj 23 waliosafiri na timu hiyo, licha ya kutoka kuoa hivi karibuni kwa kufunga ndoa na mwanamitindo na muigizaji wa filamu, Hamisa Mobetto.

Jambo hilo la Aziz Ki kuwa sehemu ya msafara wa timu hiyo, limemshtua hadi kocha Miloud Hamdi ambaye aliamini mchezaji huyo anayemiliki mabao matano na asisti saba angejipumzisha kujipongeza na mkewe, lakini mwenye wala hana mpango zaidi ni kazi kazi na hekaheka zake hazijaanzia hapo tu.

Aziz aliyeongeza mkataba mpya msimu huu, baada ya kumaliza ule wa miaka miwili uliopita amekuwa na hekaheka kabla ya hata baada ya ndoa yake na Mobetto na Mwananchi inakuletea dondoo chache kuonyesha nyota huyo raia wa Burkina Faso hana jambo dogo linapokuja suala la kuitumikia Yanga.

Licha ya sherehe ya ndoa na Hamisa, unaambiwa Aziz KI hajawahi kutegea kibaruani kwake hata siku moja, huku akihudhuria bila kujali ana jambo gani na kocha Hamdi akiendelea kumpa nafasi kikosini.

Ilianza Februari 10, ambapo alitoka Ivory Coast kuchukua baraka za ndoa kwa ndugu zake, licha ya kuwa raia wa Burkina Faso, lakini familia yake yote ipo Ivory Coast.

Inaelezwa kwamba jamaa baada ya kupata baraka hizo, alirudi nchini na kutua mjini mjini asubuhi ya siku ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya timu hiyo na JKT Tanzania iliyopigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na alianzishwa benchi kabla ya kuingia uwanjani kipindi cha pili na pambano hilo kumalizika kwa suluhu.

Baada ya hapo, Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day) yaani Februari 14, Yanga ikawa inacheza na KMC, ambapo Aziz Ki alianza kipindi cha kwanza na kufunga hat trick ya kwanza kwake msimu huu na ya pili baada ya ile ya Prince Dube pia wa Yanga.

Hat trick hiyo iliisaidia Yanga kushinda kwa mabao 6-1 na siku iliyofuata yaani Februari 15 usiku alikuwa na kazi ya kwenda kutoa mahari nyumbani kwa kina Mobeto ili kuhalalisha uchumba wao na kujiandaa kufunga ndoa.

Jamaa alitimba kwenye shughuli hiyo kama sio aliyekuwa na uchovu wa kuliamsha uwanjani na kulipa mahari kabla ya kesho yake yaani Jumapili akafunga ndoa mchana katika msikiti wa Nuur (Masjid Nuur) uliopo Mbweni.

Baada ya ndoa hiyo, hakuna aliyetarajiwa kama bwana harusi huyo angeibukia tena uwanjani katika mechi iliyopigwa Jumatatu ya Februari 17 dhidi ya Singida BS, kwani ilitarajiwa labda angekuwa fungate na mkewe, Hamisa Mobetto.

Katika mechi hiyo, Aziz Ki alianza kikosi cha kwanza na kuuwasha sana tu, sema hakuwa na bahati ya kufunga bao, kwani mabao siku hiyo yaliwekwa kimiani na Clement Mzize na Prince Dube.

Mwamba akapumzika kwa saa kama 24 tu kisha Jumatano ya tarehe 19, Februari akafanya sherehe ya harusi yao kwenye Ukumbi wa Super Dom Masaki iliyoanza usiku na kumalizika alfajiri ya juzi Alhamisi.

Unaambiwa jana Ijumaa, Aziz Ki alikuwa katika msafara wa timu hiyo kwa safari ya kwenda Kigoma ili kuvaana na Mashujaa, mechi inayopiogwa kesho Jumapili na tukio hilo la mwamba huyo kutaka kuwepo katika msafara huo, ulimshtua hadi Kocha Hamdi.

Hamdi aliliambia Mwananchi kuwa, Aziz KI ni mchezaji wa kipekee, kwani pilikapilika alizokuwa nazo nyota huyo alijiandaa kupokea maombi ya mchezaji huyo kutaka apumzike kwa safari hiyo ya Kigoma na mechi nzima ya Mashujaa kwani ikitoka hado itaenda hadi Mwanza kujiandaa kuvaana na Pamba Jiji.

“Nilijiandaa kupokea ruhusa ya Aziz KI, lakini haikuwa hivyo, kwani aliomba kukutana nami na ombi lake likawa anataka kuwa sehemu ya msafara wa timu kwenda kuipigania dhidi ya Mashujaa,” alisema Hamdi na kuongeza;

“Kiungo huyu ni mchezaji anayejitambua na nafasi yake kwenye kikosi ni kubwa akiwa uwanjani unaona kuna kitu kinafanyika hata asipofunga.

Msimu uliopita Mwamba wa Ouagadougou, ndiye aliyekuwa MVP wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 21 yaliyompa tuzo ya Mfungaji Bora wa msimu mbele ya Feisal Salum ‘Fei Toto wa Azam aliyekuwa akifukuzana naye aliyemaliza na mabao.

Related Posts