Maandalizi biashara saa 24 Kariakoo yashika kasi

Dar es Salaam. Wakati biashara eneo la Kariakoo, jijini hapa zikitarajiwa kuanza kufanyika kwa saa 24 baadaye mwezi huu, taasisi kadhaa za Serikali zinaendelea na maandalizi kuwezesha jambo hilo kutekelezwa bila usumbufu wowote.

Miongoni mwa taasisi hizo ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Wakala wa Barabarara Vijijini na Mijini (Tarura) na Mamlaka ya Udhibuti Usafiri wa Ardhini (Latra).

Tayari Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), wiki iliyopita ulisaini mkataba na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuwezesha kufunga kamera 40, shughuli itakayoanza mwanzoni mwa Machi 2025 ikiwa imetengewa Sh514.3 millioni.

Tanesco kwa sasa inabadilisha nguzo za umeme kutoka za miti kuweka za zege na kubadili nyaya za wazi za kusambazia umeme na kuweka zilizofunikwa.

Mkurugenzi Kanda ya Mashariki wa shirika hilo, Keneth Boymanda amelieleza Mwananchi kuwa kazi ya kubadili nguzo imefikia asilimia 90, huku ile ya kubadilisha nyaya ikiwa imefikia asilimia 95.

“Katika kuhakikisha lengo la Kariakoo kufanya biashara saa 24, Tanesco nasi hatujawa nyuma kuhakikisha tunashiriki ipasavyo, ikiwemo kutaka umeme nao upatikane saa 24.

“Katika kulifanikisha hilo kuna marekebisho tumekuwa tukiyafanya, yakiwemo ya kubadili nguzo na nyaya kazi ambayo tumewashirikisha kwa karibu wafanyabaiashara. Tunashukuru tulipofikia si pabaya hadi sasa, kwani tumeshakamilisha kwa kiasi kikubwa katika barabara zote zinazongia Soko Kuu la Karikaoo na baada ya hapo tutaendelea na mitaa mingine, lengo likiwa Kariakoo yote usiku uwe kama mchana,” amesema.

Hata hivyo, amesema ili kuhakikisha eneo hilo hapo baadaye halitakuwa kikwazo kwao, wameamua kuweka njia mbili za umeme ili moja itakapopata hitilafu, nyingine iendelee kufanya kazi.

“Ukiacha kuwa na njia mbili, tutakuwa na timu nne zitakazokuwa maeneo hayo kwa saa 24 ili kunapotokea dharura iwe rahisi kuishughulikia,” amesema.

Meneja wa Tarura Wilaya ya Ilala, John Magori amesema wameanza kukarabati barabara za Mtaa wa Swahili (ukarabati unaendelea), huku ya Mtaa wa Tandamti ikiwa imepata mkandarasi mwingine, hivyo muda wowote kazi itaanza.

Kuhusu taa, amesema kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji wamepanga kuweka taa 730 kuwezesha uwepo wa mwanga usiku.

Akizungumzia taa za umeme jua zinazolalamikiwa kuwa na mwanga hafifu sasa, amesema tatizo hilo wanalifuatilia.

“Kutokana na aina ya taa ambazo tumekwishaziweka maeneo mbalimbali na kuona mapungufu yake, taa zitakazowekwa safari hii niwahakikishie wafanyabaiashara na wananchi kwa ujumla, zitakuwa bora,” amesema.

Kuhusu upatikanaji wa usafiri kwa saa 24, Latra imesema italisimamia hilo kwa ukaribu kuhakikisha wananchi hawapati taabu.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Latra, Salum Pazzy amesema katika kulifanikisha hilo, maofisa wa ukaguzi watakuwepo eneo hilo saa 24.

Amesema kituo cha huduma kwa wateja cha Latra kitafanya kazi kwa saa 24, hivyo kuwa rahisi kwa abiria kutoa taarifa pale wanapofanyiwa tofauti.

Pia amesema wana mpango wa kufunga mfumo wa ufuatiliaji mwenendo wa gari (VTS) kwenye daladala zote, jambo litakalosaidia kuzifuatilia zikiwemo zinazokata ruti.

“Tunaendelea kuwasilina na wenye daladala na madereva ili kabla hatujaanza kufunga mfumo huo, tuwe tumewapa elimu. Tuna imani huko mbele itasaidia katika utoaji huduma ya usafiri,” amesema.

Kwa upande wao, Wakala wa Utoaji Huduma za Usafiri wa magari yaendayo Haraka (Udart), umesema wiki ijayo utakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumza namna ulivyojipanga.

“Nadhani mpaka Jumatatu tutakuwa katika nafasi nzuri ya kueleza namna gani tumejipanga kutoa huduma kwa saa 24, kwa kuwa leo (Februari 21) tumetoka kuongea na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhusu jambo hilo, hivyo hatuna majibu ya moja kwa moja namna gani nasi tutahudumia wananchi,” amesema Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Udart, Gabriel Katanga.

Wakati maandalizi yakiendelea, uzinduzi wa ufanyaji biashara saa 24 uliokuwa umepangwa kufanyika kesho Februari 22, umesogezwa mbele sasa utafanyika kati ya Februari 25 na 27, 2025, kwa mujibu wa Edward Mpogolo, mkuu wa Wilaya ya Ilala aliyezungumza na Mwananchi.

Januari 30, 2025 akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema uzinduzi rasmi wa biashara kwa saa 24 ungefanyika Februari 22, 2025 na shamrashamra zingeanzia ofisini kwake Ilala Boma.

Chalamila alisema ufanyaji biashara kwa saa 24 unalenga kuimarisha uchumi wa mkoa, kuongeza mapato ya Serikali na kutoa fursa za ajira.

“Tunahakikisha Mkoa wa Dar es Salaam unakuwa na mazingira bora ya kufanya biashara muda wote na tayari tunashirikiana na viongozi wa halmashauri kuimarisha maeneo yanayofaa kwa biashara za masaa 24,” alisema.

Wakati Kariakoo ikisubiri kuanza rasmi ufanyaji biashara kwa saa 24, baadhi ya maeneo ndani ya Jiji la Dar es Salaam, hasa yenye msongamano wa watu, kama vile Mbagala Rangi Tatu, Mwenge, Mbezi Luis na Buguruni biashara imekuwa ikifanyika kwa saa 24.

Hali hiyo inaonyesha kiu ya wananchi ya kufanya kazi kwa saa 24.

Wiki iliyopita Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Severine Mushi alisema wapo tayari kufanya kazi kwa saa 24 Kariakoo.

Alisema ni muhimu kufunguliwa barabara katika mitaa ya Kariakoo, ambazo baadhi zimefungwa na wafanyabiashara wanaopanga bidhaa chini (wamachinga).

Mushi alitaka kuwe na usimamizi madhubuti ili wamachinga wasifunge barabara.

Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya waendesha bodaboda na bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Said Chenja alisema moja ya maandalizi waliyoyafanya ni kuwa na sare maalumu zinazotarajiwa kugawiwa mwezi ujao.

Chenja alisema sare hizo zenye lengo la kurahisha utambuzi wa dereva, zitakuwa zinatofautiana rangi kati ya wilaya moja na nyingine, jambo litakalosaidia kujua dereva katokea eneo gani.

Related Posts