Dar es Salaam. Kuwekeza katika uongezaji wa thamani, kuongeza matumizi ya kahawa ndani ya Afrika na kuimarisha ushirikiano, ni mambo ambayo yametajwa kuwa njia zinazoweza kukuza sekta ya kahawa na kuwapa vijana fursa za ajira na maendeleo ndani ya Afrika.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa Tatu wa mwaka wa nchi zinazolima kahawa (IACO), Peosper Dodiko, wakati akitoa salamu zake katika mkutano wa tatu wa nchi 25 wazalishaji wa kahawa katika Bara la Afrika.
Katika mkutano huo, zinajadiliwa fursa zilizopo na namna ambayo vijana wanaweza kujumuishwa katika sekta ya kahawa.
Akizungumza katika mkutano huo, Dodiko ambaye pia Waziri wa Kilimo wa Burundi, amesema kaulimbiu ya mkutano huo imechaguliwa kwa umakini ili kuangazia jinsi ya kufungua fursa kwa vijana kwa kufufua sekta ya kahawa Afrika, ambayo kwa sasa haifanyi vizuri licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa ajira na maendeleo.
Amesema Afrika inajulikana kama mzalishaji wa pili wa kahawa duniani na ina idadi kubwa zaidi ya nchi zinazozalisha zao hilo, jambo linalopaswa kuonekana kama fursa.
Amesema hadi sasa, zaidi ya watu milioni 60 ndani ya Bara hili wanategemea kahawa kama chanzo cha mapato, idadi inayopaswa kuongezwa kwani rasilimali, uwezo na njia za kufanikisha hilo zipo.
“Kahawa ni zao la pili kwa thamani kubwa zaidi duniani. Kwa bara letu, sekta hii inapaswa kupewa kipaumbele,” amesema Dodiko.
Lakini tofauti na matarajio, Dodiko amesema katika miaka ya 1960, Afrika ilichangia asilimia 25 ya uzalishaji wa kahawa duniani; hata hivyo, kwa sasa uzalishaji wake ni asilimia 11 pekee.
“Hili ni pengo kubwa linaloathiri maisha ya watu wetu na fursa za ajira kwa vijana wetu. Hatuwezi kuendelea kujadili masuala ya ukosefu wa ajira na umaskini huku tukipoteza sehemu kubwa ya soko letu,” amesema.
Amebainisha kuwa kwa sasa wakulima wengi wanazeeka, hivyo ni vyema kuwapo kwa mkakati wa kuvutia vijana katika sekta hiyo.
Pia amesema wakulima wa zao hilo wanakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo hali mbaya ya hewa, mabadiliko ya tabianchi, na kushuka kwa bei za kahawa katika soko la kimataifa.
“Mkutano huu unatoa fursa ya kutathmini changamoto hizi na kuhakikisha sekta ya kahawa inakuwa endelevu na yenye faida kwa vijana wetu,” amesema.
Amesema njia moja ya kufanikisha hilo ni kuhamasisha uongezaji wa thamani katika sekta ya kahawa, kwani Afrika kwa kiasi kikubwa ni mzalishaji wa malighafi tu.
“Tunauza mazao yetu ghafi, tunapeleka ajira na kipato chetu nje ya bara letu. Ni wakati wa kubadilisha mwelekeo huu. Kwa sasa, tunasafirisha asilimia 90 ya kahawa yetu ikiwa ghafi badala ya bidhaa zilizoongezewa thamani.”
“Hii inamaanisha kwamba tunatoa nafasi kwa mataifa mengine kunufaika zaidi na juhudi za wakulima wetu. Tunapaswa kuanza kuongeza thamani kwa kahawa yetu hapa barani kwa kujenga viwanda vya kuchakata, kufungasha na kuuza bidhaa zilizokamilika,” amesema Dodiko.
Amesema serikali za Afrika zinapaswa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wengine ili kujenga vituo vya uzalishaji na uchakataji wa kahawa, jambo ambalo litaongeza ajira kwa vijana na kuimarisha uchumi wa Bara.
“Jambo lingine muhimu ni kuongeza matumizi ya kahawa ndani ya Bara la Afrika. Nchi nyingi zinazoongoza kwa uzalishaji wa kahawa, kama vile Brazil, Vietnam na Malaysia, zinatumia asilimia 36 ya kahawa yao wenyewe. Afrika inapaswa kujifunza kutoka kwao na kukuza utamaduni wa matumizi ya kahawa,” amesema.
Jambo lingine alilosisitiza ni kuhakikisha kuwa kahawa inayozalishwa Afrika inapata soko ndani ya bara kabla ya kuangalia nchi za nje, huku akisema hilo litasaidia kudhibiti bei na kuwapa wakulima kipato cha uhakika.
“Tunapaswa kushirikiana kama bara na kuzungumza kwa sauti moja katika majadiliano ya kimataifa kuhusu sekta ya kahawa. Umoja wa Afrika unapaswa kusaidia wakulima wa Afrika kwa kushawishi masoko ya haki na kuboresha miundombinu ya kifedha ili kuhakikisha sekta ya kahawa inakua kwa manufaa ya Waafrika wote,” amesema.
Mwakilishi wa Umoja wa Afrika (AU), Rebecca Teng’o, amesema bila kahawa kuchukuliwa kama bidhaa ya kimkakati ndani ya Umoja wa Afrika, Eneo la Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA) huenda lisifanye kazi kama inavyotarajiwa.