Mahakama yaamuru aliyeua kaka yake akatunzwe taasisi ya wagonjwa wa akili

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Songea imeamuru Madaha Majenga aliyekuwa akishtakiwa kwa kosa la kumuua kaka yake, Zengo Majenga kutunzwa katika Taasisi ya wagonjwa wa akili kama mhalifu mgonjwa wa akili.

Katika kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa na Jaji Emmanuel Kawishe, alitoa uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili pamoja na taarifa ya uchunguzi wa afya ya akili ya mshtakiwa.

Katika hukumu yake ya Februari 18, 2025 ambayo nakala yake imewekwa kwenye mtandao wa mahakama, Jaji alisema kwa kuzingatia taarifa ya kifo pamoja na taarifa ya uchunguzi wa akili ya mshtakiwa, inadhihirisha ni kweli alitenda kosa hilo la mauaji, lakini hakuwa na akili timamu.

Jaji Kawishe baada ya kusikia ushahidi wa pande zote mbili, alisema ni jambo lisilopingika kwamba, Zengo alifariki kwa kifo kisicho cha kawaida kilichotokana na mapigano kati yake na mtuhumiwa.

Kwa mujibu wa Jaji Kawishe, ingawa Madaha alikiri kumuua kaka yake, uchunguzi wa afya ya akili ulionesha kuwa hakuwa na akili timamu wakati wa tukio.

Alisema mshitakiwa alionyesha dalili za ugonjwa wa akili na kutokana na ripoti ya matibabu, alithibitishwa alikuwa na ugonjwa wa kichaa.

Kesi hii ilihusisha ushahidi kutoka pande zote mbili, ambapo upande wa utetezi ulileta hoja ya kwamba mshtakiwa alikuwa akiteseka na ugonjwa wa akili wakati akifanya tukio la mauaji.

Awali, wakili wa utetezi, Lazaro Simba, aliiomba Madaha akafanyiwe uchunguzi wa afya ya akili, na ombi hilo likakubaliwa na upande wa mashtaka.

Baada ya uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Isanga, ilithibitishwa kwamba Madaha alikuwa na hali ya kiakili isiyokuwa ya kawaida wakati akitenda kosa hilo.

Jaji Kawishe aatika uamuzi wake, alizingatia kifungu cha 13 cha Kanuni ya Adhabu, ambacho kinashughulikia hali ya mshtakiwa akiwa na akili timamu au la, wakati akitenda uhalifu.

Aliamua kwamba kwa kuwa mshtakiwa alikua na hali ya ugonjwa wa akili, angepelekwa kwenye Taasisi ya Isanga kama sehemu ya hatua za kisheria.

Jaji Kawishe alisema kama Madaha angepatikana na hatia ya kuua bila kukusudia, angehukumiwa kifungo cha maisha, lakini kwa kuwa alikuwa mgonjwa wa akili, alihitaji matibabu badala ya kifungo cha gerezani.

Tukio hilo lililotokea Desemba 18, 2023, lilielezewa na mashahidi, wakiwemo Dk Hassan Tambuko na Sajenti Faizi, ambao walieleza jinsi walivyofika eneo la tukio na kugundua kuwa Madaha alikuwa uchi, alionyesha dalili za ugonjwa wa akili na alikuwa akijibu kwa maneno yasiyo ya maana.

Uchunguzi wa mwili wa marehemu ulionesha kuwa alifariki dunia kutokana na majeraha ya kichwa, na kwamba alikufa kwa njia isiyo ya kawaida.

Kwa hiyo, mahakama ilikubaliana na maombi ya upande wa utetezi kwa kumtaka Madaha apelekwe kwenye taasisi ya afya ya akili kwa matibabu.

Related Posts