Na Mwandishi wetu
BARAZA la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), limeipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga misingi ya kusikiliza na kuitambua sekta hiyo katika michakato mbalimbali ya kitaifa.
Pongezi hizo zimetolewa jijini Dar es salaam leo Februari 21,2025 katika Mkutano wa kikanuni wa robo mwaka wa Baraza hilo na Mwenyekiti wa (NaCoNGO) Jasper Makala.
Makala amesema Serikali imejitahidi kuboresha mazingira wezeshi ya Mashirika hayo katika kutekeleza majukumu yao.
“Tunatoa pongezi za dhati kwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambulisha sekta hii kimataifa na kuweka diplomasia ya uwekezaji wa ruzuku na Tanzania kuonekana kwenye nchi zinazoweza kunufaika kwa ruzuku nyingi za kimataifa kwakuwa hata mijadala mingi kimataifa imekuwa ikifanyika Tanzania,”amesema Makala.
Makala amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya sita imeweza kuanzisha Jukwaa la mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (ANGOF) ambalo ni muhimu na hukutanisha wanasekta wa NGOs kila mwaka na mkakati wa uendelevu wa mashirika hayo unaosaidia kuja na mbinu mbadala kutokana na chagamoto mbalimbali za uendelevu .
Aidha amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia Mwenyekiti wa Bodi ya uratibu, Hajjat Mwantumu Mahiza ambaye amekuwa na upendo na kujua kuzisemea chagamoto za sekta ya NGO’s kwa Mamlaka mbalimbali za Serikali.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja (NaCoNGO) ilifanya ziara ya kutembelea mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliosajiliwa katika mikoa tisa Tanzania Bara ambayo ni Morogoro, Mwanza, Kilimanjaro, Mara, Geita,Kagera, Kigoma, Mbeya na Dar es salaam.
“Malengo mahususi ya zaira hii yalikuwa ni kukutanisha Mashirika haya na Mamlaka za Tawala za mikoa ili kuboresha mahusiano pamoja na kujua chagamoto ambazo wanazipitia na kupata ufumbuzi ili kuongeza ufanisi katika kusaidia wananchi wa Tanzania,”amesema Makala.