Dar es Salaam. Taarifa rasmi zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa mfumuko wa bei nchini umebakia kuwa asilimia 3.1 tangu Desemba 2024, kiwango ambacho ni chini ikilinganishwa na nchi jirani.
Katika kipindi kama hicho Kenya ilishuhudia ongezeko la mfumuko wa bei kutoka asilimia 3.0 mwezi Desemba hadi asilimia 3.3 mwezi Januari. Uganda nayo ilipata ongezeko kutoka asilimia 3.3 hadi asilimia 3.6 katika kipindi hicho.
Takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza katika udhibiti wa mfumuko wa bei ukanda wa Afrika Mashariki lakini pia kiwango cha sasa ni chini ya lengo la kitaifa la asilimia 5.
Kwa mujibu wa mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja, Tanzania imefaidika kwa kiasi kikubwa na sera thabiti za kiuchumi, hususan katika kudhibiti usambazaji wa fedha sokoni kupitia utekelezaji wa sera madhubuti za kifedha na kiuchumi.
“Kutokana na sera na sheria imara zilizowekwa na taasisi husika za kiserikali pamoja na usimamizi mzuri wa taasisi binafsi, Tanzania imeweza kupunguza shinikizo la mfumuko wa bei,” amesema Profesa Semboja ambaye ni mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Aidha, alisisitiza kuwa ni muhimu kwa mamlaka kuhakikisha zinaendelea kufuatilia na kuchambua viashiria vyote vya kiuchumi kwa umakini mkubwa ili kuepuka athari za mfumuko wa bei wa muda mrefu.
“Mara nyingi, mfumuko wa bei unapokuwa chini sana unaweza kusababisha kudorora kwa shughuli za kiuchumi na hivyo kuongeza ukosefu wa ajira mtaani. Ni lazima kuwe na uwiano mzuri kati ya udhibiti wa mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi ili kuhakikisha ustawi wa wananchi,” ameeleza Profesa Semboja.
Mhadhiri Mwingine Dk Thobias Swai, mtaalam wa masuala ya kiuchumi, alieleza kuwa serikali imekuwa na mikakati thabiti ya kudhibiti hali ya uchumi kwa ujumla.
“Uimara wa bei za mafuta, usimamizi mzuri wa sera za kifedha, pamoja na uimara wa mabadilishano ya fedha ni miongoni mwa visababishi vikubwa vinavyochangia kudhibiti mfumuko wa bei na kuuweka katika viwango vya chini,” amesema Dk Swai.