Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo ameiagiza halmashauri ya mji wa Tunduma kuwalipa wazabuni madai yao, yanayodaiwa kufika Sh1.8 bilioni tangu mwaka 2019, hali inayosababisha malalamiko mengi.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Maendeleo ya Mkoa (RCC) kwa ajili ya kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26, Chongolo ameonyesha masikitiko yake kwa hali hiyo na kuhoji sababu ya kuchelewesha malipo ya madeni hayo.
Chongolo amesema wazabuni hao walitoa huduma kwa nia njema, lakini wanakabiliwa na hali ngumu kifedha, ikiwemo kushindwa kulipa mikopo yao ya benki kutokana na ucheleweshaji wa malipo.
Amesema amewagiza wakurugenzi kuacha kuwatengenezea mazingira wafanyabiashara kufilisika huku akiwaambia kwamba wanajichukulia laana, hivyo waache kutengeneza mazingira magumu kwani hawawatendei haki wafanyabiashara.
“Lipeni madeni ya watu. Najua mlihitaji huduma hizi kwa sababu zilikuwepo kwenye bajeti, sasa hela ilienda wapi? amehoji Chongolo.
Chongolo amemtoa nje ya ukumbi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Mariamu Chaurembo pamoja na wataalamu wake ili wakae “chemba” na kupanga taarifa yao kwa mtiririko unaoeleweka na kuiwasilisha upya ili iingie kwenye kumbukumbu za kikao hicho.

Katika habari picha ni wajumbe mbalimbali wa kamati ya ushauri ya maendeleo ya Mkoa wakiwa kwenye kikao. Picha na Denis Sinkonde
“Niziagize halmashauri ya mji wa Tunduma na halmashauri nyingine katika mkoa huu kuhakikisha zinaweka mikakati madhubuti ya kulipa madeni hayo haraka ili kuimarisha uaminifu kwa wazabuni na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu katika Halmashauri ya Mji Tunduma, Emmanuel Shija ameeleza kuwa baada ya uhakiki, deni halali lililobaki ni Sh 1.01 bilioni.
Amebainisha kuwa halmashauri hiyo imeanza kulipa, ambapo Sh270 milioni zimetengwa kupitia mgawo wa fedha wa dharura (reallocation) na kwamba kwenye bajeti ya mwaka 2025 pia halmashauri hiyo imependekeza kulipa Sh370 milioni.
Hata hivyo, kupitia Ofisa Utumishi, Gilbert Mbowe ameeleza kuwa hakuna madeni ya watumishi, isipokuwa malimbikizo ya mishahara ambayo tayari yameingizwa kwenye mfumo kwa ajili ya kushughulikiwa.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wa Songwe wamepitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 ambapo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na halmashauri zake zinatarajia kukusanya na kutumia jumla ya Sh231.8 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.59 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2024/25.