Unguja. Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo imezindua mradi wa kuwaangamiza kunguru wa India ambao wanahusishwa na uharibifu wa mazao, wanyama wadogo na kuathiri uchumi wa wakulima na wafugaji.
Mwaka 1880 Serikali ya Uingereza ilipeleka kunguru hao Zanzibar kwa lengo zuri la kusaidia kupunguza takataka na mizoga mitaani, lakini idadi yao imeongezeka kwa kasi na kusababisha madhara kwa mazingira, kilimo na afya ya binadamu.
Kwa mujibu wa takwimu za wizara hiyo, mwaka 2012 walibainika kuwapo kunguru zaidi ya milioni 1.2.
Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo leo Februari 21, 2025, Waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo, Shamata Shaame Khamis, ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kunguru hao wanatokomezwa kabisa Unguja na Pemba.
“Kulingana na kampeni ya kuwaangamiza kunguru ambayo mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2012, ilibainika idadi yao walikuwa kati ya milioni 1.2. Hali hii inaleta tishio kubwa kwa bioanuwai, uchumi, afya na sekta ya utalii kwani wamekuwa waharibifu wa kula mazao na wanyama wadogo,” amesem.
Amesema mradi huo unatokana na ushirikiano uliopo kati ya wizara na kampuni ya Andrew Crow Traps Shopping Center kwa lengo la kuwaondoa kunguru hao kwa njia ya mitego maalumu, kuharibu viota, mayai, kuangamiza makinda na kuwakamata wanaonasa ili kuwaangamiza.
Shamata amesema licha ya kunguru hao kuletwa Zanzibar mwaka 1880 na Serikali ya Uingereza kwa lengo zuri la kusaidia kupunguza takataka na mizoga mitaani, idadi yao imeongezeka kwa kasi na kusababisha madhara makubwa kwa mazingira, kilimo na afya ya binadamu.
Amesema madhara ya kunguru hao ni makubwa, kwani husababisha kusambaa kwa magonjwa hatari kama kipindupindu, malaria na homa ya dengu, hivyo kwa kuwa kunguru hao hawana adui wanaoweza kuwawinda na kupambana nao, kutoweka kwao kunategemea zaidi vifo vya kawaida.
Awali, mtaalamu wa kutengeneza mitego hiyo, Andrew Mbena kutoka kampuni ya Andrew Crow Traps Shopping Center, amesema idadi ya kunguru milioni 1.2 ni kwa mujibu wa makadirio ya mwaka 2012, ambayo kwa sasa inakisiwa kuongezeka maradufu.
“Baada ya kampeni ya 2012 hadi sasa, kunguru hawakupata msukosuko wowote wala hakukufanyika zoezi la kuwaondoa kwa muda wote huo, hivyo ni lazima idadi yao itakuwa imeongezeka hata mara tatu,” amesema.
Mtaalamu huyo ameiomba Serikali na taasisi binafsi kuwasaidia na kuwapa ushirikiano kupitia kampeni ya kuwaangamiza kunguru hao.
Mkurugenzi Idara ya Misitu Zanzibar, Said Juma Ali, ametoa wito kwa wadau wote kushiriki kwa kuchangia vifaa, fedha na mawazo ili kufanikisha programu hiyo.
“Hadi sasa tunatumia rasilimali za ndani kuendesha programu hii kwa ajili ya kuangamiza kunguru. Kwa hiyo, ushiriki na msaada wenu unahitajika sana. Pia wenye uwezo wa kutengeneza mitego wajitolee ili iongezeke nchini,” amesema.
Amesema programu hiyo itafanyika Zanzibar nzima ikianzia Unguja kwa sasa, akiwataka wananchi kutoa ushirikiano ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Hata hivyo, amesema programu hiyo haitahusisha watoto wadogo na tayari mitego mitatu imewekwa katika maeneo manne ambayo ni ofisi ya wizara hiyo, Idara ya Misitu na Shakani. Hivi karibuni wataweka mitego minne katika Hospitali ya Mkoa Lumumba.
Wakizungumzia hatua hiyo baadhi ya wananchi na wajasiriamali kisiwani Unguja wameipongeza, wakieeza madhila wanayopitia kutokana na ujasiri wa ndege hao.
“Kunguru ni wakorofi, wanakuja wanakula mchele waziwazi hata ukimfukuza wanadharau sana, kwa hiyo binafsi napongeza kama kweli wataangamizwa na sisi tutasaidika,” amesema Kassim Haji, ambaye ni mjasiriamali.
Khadija Khamis, mkazi wa Gulioni amesema: “Hawa kunguru hata ukiwa unatengeneza kitoweo wanachukua bila woga, wamekuwa wengi bora waangamizwe.”