Serikali kutathimini ulazima kampuni za simu kuuza hisa

Arusha. Serikali imesema ipo tayari kurudi kwenye meza ya mazungumzo na wadau wa sekta ya mawasiliano kutathimini utekelezaji wa sheria inayozitaka kampuni za simu kuuza asilimia 25 ya hisa zake kwa umma, kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Mpaka sasa ni Vodacom Tanzania pekee iliyotekeleza takwa la Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Epoca) ya mwaka 2020 na Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 zinazotaka kampuni za mawasiliano ya simu kujisajili na kuuza asilimia 25 ya hisa zake kwa umma kupitia DSE. Kampuni nyingine zimekuwa zikisema kuwa zinaendelea na mchakato.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema hayo jana Alhamisi Februari 20, 2025 kwenye kikao kazi cha watendaji wa wizara hiyo na wadau kujadili utekelezaji wa mkakati wa miaka 10 wa uchumi wa kidijitali (2024 hadi 2034).

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema Serikali ipo tayari kurudi kwenye meza ya mazungumzo na wadau kutathmini utekelezaji wa Sheria hiyo iliyotungwa mwaka 2017.

Amesema kuna changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa sheria hiyo licha ya hatua zilizochukuliwa na kampuni za simu ikiwemo Vodacom na kwamba, bado kuna masuala yanayohitaji marekebisho.

Silaa amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau, itafanya tathmini ya hatua zilizochukuliwa hadi sasa ili kuboresha utaratibu na kuhakikisha sekta ya mawasiliano inakua na tija na faida kwa pande zote.

“Napata maswali mengi, lini wengine watajiunga, lakini vilevile kwa maelezo yako performance ya wale waliotangulia haijawa nzuri. Nadhani njia bora zaidi ya kukuza sekta yoyote kwenye uchumi huu wa soko ni kuacha sekta zitawaliwe na nguvu ya soko.

“Tukianza kutengeneza shuruti kwenye baadhi ya mambo matokeo yake ndiyo haya, unachosema sina tathmini sahihi lakini, ndiyo hicho ulichokisema. Nadhani ni wakati sahihi sisi kama Serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwa sababu tuna wadau, tutakaa tuangalie tulipotoka, maamuzi tuliyoyafanya, tulipo ili tutengeneze utaratibu mzuri huko tunapokwenda,” amesema Silaa.

Amesema ni wakati mwafaka kwa Serikali na wadau kukaa ili kutengeneza njia bora zaidi ya kampuni hizo kujiendesha kwa kuweka miongozo yenye kukidhi matarajio ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Sheria tunazitunga ili kurahisisha mambo kwa utaratibu, sio kutufunga kwa kuwa sheria si msaafu. Wabunge wapo hapa, Kamati ya Bunge ipo. Nadhani ni wakati muafaka wa sisi kukaa na kutengeneza njia bora zaidi kwa kampuni hizi kujiendesha,” amesema Silaa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari, hivi karibuni aliliambia gazeti la The Citizen kuwa hitaji la kisheria la kampuni za mawasiliano kuorodheshwa DSE bado lipo, na kwamba kampuni husika zipo katika hatua tofauti za mchakato huo.

Kwa mujibu wa kanuni za DSE, kampuni zilizo kwenye soko la hisa zinatakiwa kuchapisha taarifa zakr za kifedha za kila mwaka, hatua inayoiwezesha Serikali na umma kwa ujumla kuelewa hali ya kifedha ya kampuni hizo kwa uwazi zaidi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya udalali wa hisa, Zan Securities, Raphael Masumbuko amesema uwazi huo ni muhimu kwa tathmini sahihi ya kodi na kuhakikisha utekelezaji mzuri wa sheria za mapato, jambo linalosaidia kuwa na mfumo wa mapato wa haki zaidi,

Alisema kuwa msingi wa hitaji la kisheria la kampuni za mawasiliano kuorodheshwa DSE unatokana na ukweli kwamba wanahisa wake wakubwa ni wageni, hivyo kulazimika kuuza sehemu ya hisa zao kupitia soko la ndani ili wananchi pia wanufaike.

“Kampuni zilizo kwenye soko la hisa zinaweza kuwa miongoni mwa walipa kodi wakubwa kutokana na kuongezeka kwa ufanisi na uwazi,” alisema Masumbuko.

Related Posts