SERIKALI YAENDELEA KUPIGA HATUA KATIKA KULINDA HAKI ZA BINADAMU KATIKA BIASHARA

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mohamed Khamis Hamad akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mapitio ya mpango kazi wa haki za binadamu na biashara, kikao kazi hicho kimefanyika jijini Dar es Salaam leo Februari 21,2025.

Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha, Noel Komba akizungumza na waandishi wa habari namna mpango kazi wa haki za binadamu na biashara utavyonufaisha. Kikao kazi hizo kimefanyika jijini Dar es Salaam leo Februari 21, 2025.

KATIKA jitihada za kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa ipasavyo katika shughuli za kibiashara, Serikali kupitia Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Uandaaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara imefanya kikao muhimu cha mapitio ya Rasimu ya Mpango huo.

Katika kikao hicho, Timu ya Wataalam imekabidhi Rasimu ya awali kwa Kamati kwa lengo la kufanya maboresho na kuidhinisha mpango huo kabla ya hatua za mwisho za utekelezaji. Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mohamed Khamis Hamad jijini Dar es Salaam leo Februari 21, 2025 amesema mpango huo ni hatua muhimu katika kuhakikisha biashara zinaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu.

Mpango kazi huo umechangiwa na wadau kutoka taasisi za serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia, na wataalam wa masuala ya haki za binadamu na biashara, huku ukilenga kuhakikisha kuwa sekta ya biashara inakua kwa uwiano wa kuheshimu haki za wafanyakazi, jamii, na mazingira wanayofanyia kazi.

Kwa mujibu wa Hamad, serikali tayari imeonyesha dhamira ya kuusimamia mpango huu, ambapo baada ya rasimu kukamilika, utawasilishwa kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa pande zote za Tanzania Bara na Zanzibar ili kuratibu hatua za mwisho kabla ya utekelezaji rasmi.

Kwa upande wake, Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha, Noel Komba, amesema mpango huo utafungua milango ya uwekezaji zaidi kwa sababu unaleta mazingira ya kibiashara yenye utulivu na haki kwa wawekezaji na wafanyakazi. Ameeleza kuwa utachochea maendeleo katika sekta za viwanda, utalii, kilimo na biashara kwa ujumla, huku ukiimarisha uwajibikaji wa makampuni kwa jamii inayozunguka shughuli zao.

Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara unatarajiwa kuwa nyenzo muhimu ya kutekeleza maazimio mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo Miongozo ya Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Binadamu. Serikali inatarajia kukamilisha hatua za mwisho za maandalizi na kuanza utekelezaji wake kabla ya mwaka 2030.

Hatua hii inatoa taswira ya maendeleo ya kidemokrasia na kimaadili katika biashara, huku Tanzania ikijiweka katika nafasi nzuri ya kuvutia uwekezaji wa ndani na nje unaozingatia viwango vya haki za binadamu.

Related Posts