Silaa: Kila mtu ana wajibu wa kujilinda utapeli mtandaoni

Arusha. Serikali imesema kila mwananchi ana wajibu wa kujilinda dhidi ya utapeli na ulaghai wa mtandaoni ikiwemo kutotoa taarifa zake binafsi kwa mtu asiyemfahamu.

Pia, imesema wengi waliotapeliwa wametoa taarifa zao binafsi ikiwemo kutoa nywila zao kwa vyanzo mbalimbali na kujikuta wametapeliwa.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Februari 21, 2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi cha sekta hiyo, ikiwa siku moja baada ya kuzindua kampeni maalumu ya kupambana na utapeli mitandaoni, ijulikanayo kama ‘Sitapeliki’.

Waziri huyo amesema mdau mkubwa wa ulinzi na kujihadhari ya utapeli au ulaghai wa mtandao ni mwananchi mwenyewe, hivyo kila mtu ana wajibu wa kuongeza juhudi za kujilinda.

Amesema ulinzi uliokuwa unawekwa wakati hakuna matumizi makubwa ya fedha kidijitali, unapaswa kuwekwa kwenye simu zao.

“Zamani ulikuwa unaenda benki unatoa Sh1 milioni yako ukirudi nyumbani unaifungia kwenye kabati unaweka na kufuli au sefu, leo Sh1 milioni yako iko kwenye simu, lazima ulinzi unaoufanya kwenye simu yako uwe kuanzia kwenye simu yenyewe na namba yako ya siri.

“Niwaombe sana ma-admin kwenye makundi ya mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp na watumiaji, tuelimishane kuhusu tahadhari za utapeli wa mitandaoni. Huko mtandaoni tengenezeni mjadala wa kuelimishana kwa sababu inawezekana mtu haangalii televisheni au hasikilizi redio, lakini yuko na simu yake,” amesema.

Amesema Novemba 22, 2024 walikaa kikao cha wadau wa mawasiliano kwa lengo la kutafuta mwarobaini wa utapeli mtandaoni kwani namna teknolojia inavyoongezeka, ndivyo vitendo hivyo vinaongezeka.

Waziri Silaa amesema ni muhimu wananchi kutambua kuwa wakitapeliwa wakatoa taarifa katika vituo vya polisi na kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani imeendelea kuwanoa makachero wake ambao watafanya kazi ya kushughulikia kesi hizo.

“Ili kuwasiliana na mteja, kampuni zote za simu zinatumia namba ya huduma kwa wateja 100, mwananchi asipigiwe simu na mtu kwa namba ya kawaida na akaambiwa yeye ni mtoa huduma, kwani wanaotumia namba tofauti na 100 ni matapeli,” amesema.

“Tutaenda kuona jinsi gani watoa huduma wanakuwa na chaneli zao za mitandao ya WhatsApp ambayo haiwezi kukutumia ujumbe mfupi hadi utakapoifuata, ambapo watoa huduma wataona namna wananchi watapewa taarifa na watoa huduma hao.

Waziri Silaa amesema Watanzania wana wajibu wa kutambua wakipoteza laini zao za simu wanapaswa kutoa taarifa kwa watoa huduma wao ili zisije kutumika vibaya ikiwemo kutapeli watu wao wa karibu.

“Mtu ana simu ndogo ya Sh20,000, ikipotea anaona kama vile aachane nayo na asajili laini nyingine. Ile simu ikiokotwa na ikiwa haina namba ya siri, ikifunguka mtu anaangalia simu gani umepiga mara ya mwisho, anaanza kuwatumia ujumbe na kuwatapeli,” ameongeza.

Related Posts