Siri ya mama kumtazama mtoto anaponyonyesha

Dar es Salaam. Mama mjamzito anapojifungua mtoto salama ama kwa njia ya kawaida au upasuaji,  hatua inayofuata huwa ni tendo la unyonyeshaji.

Hatua hiyo ni muhimu  katika maisha ya mtoto kwani  wataalam wa afya na lishe kote duniani, wanakubaliana kuwa unyonyeshaji ni mojawapo ya njia bora zaidi za kuhakikisha ukuaji na uimara wa afya ya mtoto kimwili na kiakili.

Maziwa ya mama yanatajwa kuwa na viinilishe vyote muhimu vinavyomsaidia mtoto kukabiliana kwa ufanisi mkubwa dhidi ya maambukizi ya vimelea vya magonjwa.

Pamoja na kumpatia mtoto lishe bora, mchakato huu unasaidia kujenga uhusiano wa karibu kati ya mama na mtoto.

Kitaalamu wakati wa tendo la unyonyeshaji,  mama anashauriwa kumuangalia mtoto usoni, Hata hivyo baadhi ya wanawake wamekuwa wakiwanyonyesha watoto wao huku wakiendelea na shughuli nyingine kama vile kuangalia televisheni, kuperuzi katika mitandao ya kijamii au kuzungumza na watu wengine.

Baadhi ya mama hufanya hivyo kutokana na kutojua umuhimu wa kupata utulivu na kumuangalia mtoto wakati wa kunyonyesha.

Aisha Juma mkazi wa Makulu jijini Dodoma na mama wa watoto wawili, anasema huwa hazingatii jambo hilo kutokana na kutojua umuhimu wake.

“Ninachozingatia ni mtoto amekaa katika mkao sahihi ambao unamfanya aweze kunyonya vizuri. Sikuwahi kufahamu kama kuna umuhimu wa kumnyonyesha mtoto huku ukimtazama usoni”anaeleza.

Pia Scolastica Kivaula mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam mama wa mtoto mmoja anasema anapomnyonyesha mtoto wake,  huwa anazingatia kumtazama usoni huku akitabasamu kwa kuwa wanaelekezwa hospitalini kuwa inasaidia kujenga ukaribu kati ya mama na mtoto.

“Katika madarasa ya unyonyeshaji niliyowahi kushiriki kwa njia ya mtandao,  suala hilo huwa linasisitizwa kuzingatia kutokana na umuhimu wake katika ukuaji wa mtoto”anaeleza.

Nae Amanda Rashid anasema huwa anajisikia furaha pale anapomnyonyesha mtoto wake huku akimtizama usoni na kumuona akitabasamu.

“Yani hata kama nilikuwa nina changamoto fulani inanikabili, ninapomuona mtoto wangu akitabasamu wakati ninamnyonyesha huwa inanipa faraja”anaeleza.

Kutozingatia hilo kunatajwa na wataalamu kunaweza kusababisha kupunguza ukaribu na upendo kati ya mama na mtoto pamoja na kuathiri ubongo wa mtoto.

Kwa mujibu wa tovuti ya Milkcollective mtoto anapozaliwa na punde kuanza kunyonya ziwa la mama huku wakitazamana usoni, hali hiyo inamsaidia mtoto kuifahamu vyema sura ya mama yake ndani ya siku nne.

Vilevile inaeleza kuwa haijalishi mtoto ananyonya ziwa la mama au kwa kutumia chupa, mama anapaswa kumtazama usoni mtoto wake kwa ukarimu na tabasamu kwani kufanya hivyo kunatengeneza msingi mzuri wa mawasiliano kati ya mama na mtoto.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa mkunga msaidizi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bahi, Anitha Mganga,  anasema inaweza kuonekana kama tendo dogo,  lakini ndicho kipindi ambacho mtoto hujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa mama.

Mganga anasema kumuangalia mtoto usoni wakati wa kunyonyesha husaidia katika kuimarisha uhusiano wa kihisia kati ya mama na mtoto.

“Mtoto anapohisi upendo na uangalizi wa mama kupitia kutazamana machoni,  hujenga hali ya kuaminiana na usalama, jambo linalosaidia katika ukuaji wake wa kihisia”

“Wakati mama anamwangalia mtoto wake usoni, kuna muunganisho wa kihisia unaojengwa. Mtoto anahisi kupendwa, kuthaminiwa na kuwa salama”anasema.

Anaongeza kuwa wakati wa unyonyeshaji,  watoto hupendelea kuhisi upendo na kujaliwa na mama.

“Hiyo ndiyo sababu wakati mwingine mtoto akiona mama hamzingatii humng’ata kwenye chuchu kama njia ya kumkumbusha kuwa anahitaji umakini wake”anaeleza.

Vilevile anaeleza kuwa kwa kufanya hivyo inasaidia kuimarisha maendeleo ya ukuaji wa ubongo wa mtoto.

Aidha, anasema mawasiliano ya macho kati ya mama na mtoto wakati wa kunyonyesha, huchochea ukuaji wa ubongo wa mtoto.

“Tafiti zinaonyesha kuwa watoto wanaopokea mwingiliano wa kihisia na mama zao, wanakuwa na maendeleo mazuri ya kiakili na wanakuwa na uwezo mzuri wa kujifunza”anaeleza.

Kwa upande wake,  Meneja mradi wa afya ya mama na mtoto na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Word Vision, Dk Daud Gambo anasema kitendo cha mama kumtaza mtoto usoni wakati wa unyonyeshaji,  humuhamasisha mtoto kunyonya vizuri.

Vilevile anasema inamsaidia mama kugundua mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida kwa mtoto wake.

“Mama anapomwangalia mtoto wake usoni, anaweza kuelewa iwapo mtoto anaendelea kunyonya vizuri, kama ana furaha au anapitia changamoto fulani,”anaeleza.

Related Posts