Uvuvi kupindukia kikwazo Zanzibar | Mwananchi

Zanzibar. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, imesema uvuvi kupindukia ni miongoni mwa changamoto za bahari visiwani humo.

Imesema idadi ya wavuvi visiwani humo ni kubwa na wengi wao hufanya shughuli hiyo katika maeneo ya karibu ya bahari jambo linalosababisha athari za kimazingira baharini.

Akizungumza katika jukwaa la kwanza la usimamizi  Bahari na Pwani (Tanzania Chapter Ocean Governance Forum) leo Ijumaa Februari 21, 2025, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Zahor Kassim Elkharousy, amesema shughuli za uvuvi visiwani humo zinafanyika  kupindukia, jambo linalosababisha changamoto za kimazingira za bahari.

“Tuna wavuvi wengi, jambo linalosababisha kuwe na changamoto ya uvuvi uliopindukia, bahati mbaya wavuvi wengi wanafanya shughuli za uvuvi katika maeneo ya karibu.

“Katika kukabiliana na hili, Serikali inawapa wavuvi vifaa ili kuwawezesha kufanya shughuli hizo katika maeneo ya mbali,” amesema.

Amesema bado kuna changamoto katika masuala ya uharibifu mazingira habarini ikiwamo kukata miti ya mikoko ambayo ni muhimu.

Akizungumzia jukwaa hilo, amesema litasaidia kukabiliana na changamoto hizo na zingine zinazoikabili bahari.

“Sote tunafahamu bahari ina mtumizi mengi si uvuvi pekee, kuna mafuta na gesi, madini, usafirishaji na shughuli nyingine, wadau wa sekta hizi kama wakifanya kazi kwa ushirikiano tutapanua wigo katika matumizi sahihi na uhifadhi wa bahari yetu,” amesema.

Elkharousy aliyekuwa mgeni rasmi katika jukwaa hilo amesema kuimarishwa kwa mifumo ya usimamizi wa bahari kutasaidia uvuvi endelevu, utalii, na biashara ya baharini kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumzia umuhimu wa jukwaa hilo, Naibu Katibu – Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Christina Mndeme amesema litasaidia kuendesha sera zinazotokana na ushahidi wa kisayansi na suluhisho jumuishi.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi  na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Immaculate Sware  alisema bado bahati haijatumika inavyotakiwa na kubainisha matumizi ya bahari kwa sasa ni kwa asilimia 10 pekee.

Amesema rasilimali za bahari nchini Tanzania ni nguzo muhimu kwa ukuaji wa uchumi, usalama wa chakula na uhifadhi wa mazingira.

“Hata hivyo, changamoto kama uvuvi kupita kiasi, uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa makazi ya viumbe wa baharini na mabadiliko ya tabianchi zinaathiri ustawi wa mifumo hii ya ikolojia,” amesema katika jukwaa hilo mahususi kwa ajili ya mabadiliko, kuhamasisha ushirikiano wa wadau mbalimbali, kuoanisha sera, na kubuni suluhisho bunifu kwa usimamizi endelevu wa bahari.

Jukwaa hilo lilimeandaliwa NEMC kwa ushirikiano wa mashirika ya Serikali, taasisi za elimu, washirika wa maendeleo, sekta binafsi, na mashirika ya kijamii.

Related Posts