Unguja. Miundombinu hafifu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika sekta hiyo vimeelezwa kuchangia uzoroteshaji wa utoaji huduma licha ya kupiga hatua katika sekta ya afya, kukosekana kwa wataalamu wenye sifa.
Changamoto hizo pia zinachangia kukosekana uwekaji wa kumbukumbu za taarifa za afya na kuifanya Serikali ikose takwimu za kuaminika wakati wa kufanya uamuzi katika sekta hiyo.
Hayo yamebainika katika mkutano wa 14 wa mapitio na mpango wa pamoja wa utekelezaji wa sekta ya afya Februari 21, 2025 kisiwani Unguja.
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya upungufu wa wataalamu wenye sifa na miundombinu ya Tehama.
“Haya yanachangia kuzorotesha kasi ya utoaji huduma na uwekaji wa kumbukumbu, hivyo Serikali kushindwa kufanya uamuzi sahihi,” amesema.
Kwa mantiki hiyo, amesema Wizara ya Afya itahakikisha inaweka mfumo wa kidijitali unaosomana katika ngazi zote za utawala na utoaji wa huduma ambao utawezesha kupata takwimu sahihi zitakazosaidia kufanya uamuzi kwa uhakika.
Amesema Serikali itaendelea kufanya jitihada kwa kushirikiana na wadau wa afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa vituo vya afya na hospitali, ikiwemo kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
Hata hivyo, amesema Serikali imepata mafanikio makubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi, ikiwemo kuimarika kwa huduma za uchunguzi wa maradhi, huduma za wagonjwa mahututi, kuongezeka kwa kiwango cha chanjo kwa watoto na kuongezeka hospitali zenye uwezo wa kutoa huduma za matibabu ya watoto njiti.
Nyingine ni huduma za mama na mtoto na huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, zikiwemo za upasuaji na usafishaji figo.
Kwa mujibu wa Hemed, Serikali imehakikisha mitambo ya kuzalishia hewa tiba imeimarika pamoja na kuimarika kwa afya ngazi ya jamii, ikiwemo kuanzisha mifumo ya uendeshaji na usimamizi wa taarifa za wanachama wa Mfuko wa Huduma za Afya (ZHSF) na Mfuko Maalumu wa Maendeleo ya Afya Zanzibar (ZDF).
Amewataka watoa huduma za afya kuendelea kuzingatia maadili na kufanya kazi kwa bidiii na nidhamu ya hali ya juu ili kupunguza malalamiko yanayotolewa na wananchi dhidi yao.
Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui amesema wizara inaendelea kuimarisha huduma za Afya ya Msingi (CHW) kwa kuboresha miundombinu ya upatikanaji wa huduma bora.
“Serikali inaendelea kujenga hospitali, vituo vya afya na makazi ya wafanyakazi wake ili kusogeza karibu na wananchi huduma bora za afya, zitakazosaidia kuondoa changamoto kadhaa, ikiwemo vifo na kuongezeka kwa maradhi hasa yasiyoambukiza,” amesema.
Mwenyekiti wa Washirika wa Maendeleo ya Afya na Lishe Zanzibar, Laxmi Bhawawi ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira rafiki kwa wadau wa sekta ya afya kwa kujenga hospitali na vituo vya afya katika kila wilaya na mkoa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
Bhawawi amesema washirika wa maendeleo wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kufikia malengo ya kutoa huduma bora za afya kwa jamii.
“Tutaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha inaweka mipango madhubuti kwa maendeleo ya sasa na baadaye kwa kuimarisha sekta ya afya,” amesema.