Yanga yatiwa hasira Ligi Kuu

YANGA inapaa leo kwenda Kigoma ikiwafuata wanajeshi wa Mashujaa, lakini kocha wa timu hiyo, Hamdi Miloud amewajaza upepo washambuliaji Prince Dube na Clement Mzize akiwaambia waamue wao kwani kiatu cha ufungaji bora kipo kwenye miguu yao.

Kwenye msimamo wa ufungaji kinara wa mabao ni Mzize amefunga 10 sawa na kiungo wa Simba Jean Charles Ahoua na nyuma yao yupo Dube mwenye tisa.

Msimamo huo ukamuibua Hamdi aliyeliambia Mwanaspoti washambuliaji hao wanamkosha kwa namna wanavyoendelea kutikisa nyavu akisema maamuzi ya kupata kiatu hicho yapo kwenye miguu yao.

Miloud alisema katika kikosi hicho uhakika ni nafasi za kufunga zitakuwa nyingi kutokana na falsafa yao ya kushambulia kwa kasi na wao wanatakiwa kuongeza utulivu wa kutumia nafasi hizo.

“Wanafanya vizuri sana Clement (Mzize) na Dube (Prince) ukitazama wanaonyesha njaa ya kutaka kufunga lakini kitu kizuri zaidi wanacheza kwa ushirikiano mkubwa baina yao unaona namna wanatengenezeana nafasi za kufunga,” alisema Hamdi anayeaanza mechi za ugenini mikoani dhidi ya Mashujaa.

“Kitu wanatakiwa kukifanya sasa ni kuongeza utulivu wa kutumia nafasi kwa kuwa kama unavyoona timu inawapa uhakika wa huduma ya nafasi, wakiongeza umakini wanaweza kuchukua wote kiatu cha ufungaji bora au mmoja wao,” alisema Hamdi na kuongeza;

“Unapokuwa katika timu bora kama hii yenye viungo wabunifu unapata uhakika wa kufanya makubwa kwenye kufunga kama ambavyo wanaendelea kufanya lakini kwangu mimi nataka wafunge zaidi na kuendelea kusaidiana.”

Aidha Hamdi amewapongeza pia viungo wake kwa namna wanavyoendelea kuonyesha ubora kwenye mechi zao huku pia wakiwa sawa kwenye kufunga.

“Kila mchezaji anajukumu la kuwa sehemu ya kutengeneza ushindi wa timu, nafurahia pia jitihada na ubunifu wa viungo wetu wanafanya kazi nzuri unaona wakipata nafasi wanatengeneza mabao lakini pia kuna wakati nao wanafunga kwa kuwa wanaweza kufanya hivyo.”

Related Posts