Dar es Salaam. Serikali imesema watu 93 waliohisiwa kuwa na dalili zinazofanana na ugonjwa wa marburg, wameruhusiwa baada ya kupimwa kwa kuzingatia taratibu na kanuni za afya ya kimataifa na kuthibitika kuwa hawana virusi vya ugonjwa huo.
Tangu Januari 20, 2025 Serikali ilipotoa taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa wa virusi vya marburg (MVD) mkoani Kagera, idadi ya wagonjwa waliothibitishwa ni wawili ambao walikwishafariki dunia.
Taarifa iliyotolewa leo Februri 22, 2025 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe imeeleza kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi na wadau, wameendelea kufanya ufuatiliaji wa kina.
“Tumefanya ufutiliaji kwa watu wenye viashiria vya ugonjwa kwenye jamii na vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo wahisiwa 93 wenye dalili zinazofanana na ugonjwa wa marburg walipimwa kwa kuzingatia taratibu na kanuni za afya ya kimataifa na kuthibitika kuwa hawana virusi vya Marburg,” amesema.
Amesema kwa mujibu wa taratibu za udhibiti wa magonjwa za kimataifa, wale wote waliotangamana na wagonjwa waliwekwa mahali maalum ‘karantini’ na kufuatiliwa kwa kipindi cha siku 21 na wamethibitika kutokuwa na maambukizi na sasa wameruhusiwa na wanaendelea na shughuli zao za kawaida.
Dk Magembe amesema Serikali inaendelea na mikakati ya kudhibiti ugonjwa huu ambapo mgonjwa wa mwisho kugundulika ilikuwa Januari 28, 2025 na kwamba hadi sasa siku 23 zimepita bila uwepo wa mgonjwa aliyethibitika kuwa na ugonjwa wa marburg wala kifo.
Aidha amesema Serikali imeendelea kutoa elimu juu ya dalili, madhara pamoja na njia za kujikinga.
Pia, amekumbusha kuwa, nchi inaendelea kukabiliwa na tishio la magonjwa mengine ikiwemo ebola na homa ya nyani (Monkeypox) yanayoendelea katika nchi mbalimbali duniani.
Magonjwa hayo huambukizwa na kusambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa kugusana na majimaji yaliyotoka kwa mgonjwa mwenye maambukizi ya virusi vya ugonjwa husika.
Katika hatua nyingine, Wizara imewakumbusha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu, unaoendelea kuripotiwa katika baadhi ya maeneo nchini.
Amesema ugonjwa huu kwa sehemu kubwa unadhibitiwa kwa kuzingatia kanuni za afya na usafi wa mazingira kwa kutumia maji safi na salama, kuepuka kula matunda bila kusafisha, kula chakula cha moto na kuimarisha usafi wa mazingira na matumizi sahihi ya vyoo.
“Wizara inatoa rai kwa wataalam wa afya katika ngazi zote nchini, kuimarisha uchunguzi wa awali wa dalili za magonjwa haya katika vituo vyote vya kutolea huduma na kuimarisha zaidi utoaji wa elimu kwa umma juu ya namna ya kujikinga, kutambua na kubaini wahisiwa wa magonjwa haya katika jamii,” amesema.
Dk Magembe ametoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano na kuzingatia kanuni za afya za kinga na udhibiti kadri zinavyotolewa kupitia matangazo na njia zingine.
Jinsi ya kujikinga Dk Magembe amewataka wananchi kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu iwapo watakuwa na dalili za homa, uchovu wa mwili, kutapika au kuharisha damu au kutoka damu maeneo mbalimbali ya mwili.
Kutoa taarifa kwa haraka kwenye kituo cha kutolea huduma kilicho karibu au kupiga simu namba 199 bila malipo endapo utamuona mtu mwenye dalili hizo.
Kuepuka kumgusa mgonjwa au majimaji ya mwili bila kinga mfano mate, machozi, damu, mkojo na kinyesi yatokayo kwa mgonjwa au mtu yeyote mwenye dalili zilizotajwa hapo juu.
Kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono na epuka kusalimiana kwa kushikana mikono.
“Kwa kuchukuwa hatua hizi na kuzingatia ushauri wa wataalamu, tunaweza kujikinga dhidi ya marburg, ebola, na monkeypox,” amesema Dk Magembe.