Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, leo Februari 22, 2025, amefanya mabadiliko ya kiutendaji katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA).
Kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5/2019, Waziri Aweso amemteua CPA Sais Andongile Kyejo kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA.
Kyejo alikuwa Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na sasa atachukua nafasi ya Mhandisi Tamimu Katakweba, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA.
Aidha, Waziri Aweso amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, kuunda timu maalumu ya wataalamu watakaoshughulikia changamoto za upatikanaji wa maji katika Manispaa ya Morogoro na maeneo yote yanayohudumiwa na MORUWASA, wakati utekelezaji wa Mradi Mkubwa wa Maji ukiendelea.