Mbeya. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimesema licha ya manung’uniko lakini kipo tayari kwa uchaguzi mkuu, huku kikitaka kura ya mwananchi iheshimiwe.
Pia, amesema chama hicho kimesikitishwa na uchakavu wa miundombinu ya barabara katika mitaa ya Jiji la Mbeya huku akiitupia lawama CCM kwamba hakijawa tayari kuwatumikia wananchi ipasavyo.
Akizungumza leo Februari 22, 2025 katika ziara yake ya kwanza mkoani hapa, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Hashim Rungwe amesema yapo manung’uniko kufuatia uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27 mwaka jana akieleza kuwa haukuwa wa haki.
Amesema pamoja na manung’uniko waliyonayo kama ilivyo kwa vyama vingine vya upinzani, lakini Chaumma kipo tayari kwa uchaguzi akieleza kuwa CCM inapaswa kuheshimu kura za wananchi kwani ndio wenye mamlaka ya kuweka kiongozi madarakani.
“Inashangaza sana, mtu anapoumwa hapati huduma anasubiri ndugu, jamaa au rafiki kupata msaada wa chakula, mimi mwenyewe nimeumwa sikupata chakula hospitali, lazima mgonjwa apate hiyo anapokuwa hospitali.

“Wakati nikiwa shule tulipewa chakula, maziwa na kila kitu ilikuwa bure, lakini kwa sasa mnatozwa gharama, hizi fedha zimeelekezwa kuwaajiri wakuu wa wilaya ambao hawana kazi yoyote” amesema Rungwe.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa wananchi wanalipa kodi, lakini miundombinu si rafiki akieleza kuwa CCM inaandaa njia inapotokea ugeni aidha wa Rais na kwamba hali hiyo ni kutoheshimu wananchi.
“Kuhusu ofisi ya mkoa, katibu mkuu atalishughulikia na tutalifanyia kazi, niwahakikishie Chauma kitabaki kuwa imara wakati wote, hivyo tunaomba wakati wa uchaguzi mkuu tupeni kura,” amesema kiongozi huyo.
Mwenyekiti wa Wanawake wa chama hicho Taifa, Verena Marwa amesema bado hawajaona mabadiliko katika uchaguzi akieleza kuwa kero ya maji na umeme ni changamoto.
Hata hivyo, ametumia muda huo kushukuru wananchi katika Mtaa wa Soko jijini Mbeya waliompa kura Mwenyekiti wa Chama hicho, Brayan Mwakalukwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kumtambulisha rasmi kwa wananchi.
“Niwapongeze na kuwashukuru wananchi kwa kukiheshimisha chama chetu, tunahitaji uchaguzi mkuu madiwani na wabunge tuchukue maeneo mengi,” amesema Verena.
Naye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Issa Abas amesema wanapongeza ushindi huo akieleza kuwa siasa si vita wala uhasama kama baadhi ya vyama wanavyoamini.
“Malengo yetu ni kuona Chaumma kinashika dola ili kuwapa maendeleo wananchi, sisi tunahitaji amani ya nchi, kwa niaba ya Zanzibar tunashukuru na kupongeza ushindi huu,” amesema Abas.
Akizungumza kwa niaba ya vyama vingine, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM, Mkoa wa Mbeya, Christopher Uhagile amesema wanaamini katika demokrasia na ndio maana mtaa huo waliweza kupoteza katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Hii ndio sera ya CCM na utekelezaji wa 4R za Rais Samia (Rais Samia Suluhu Hassan), huu mtaa ulitutoa jasho na kwa sasa tunaamini Chaumma ndicho chama kikubwa cha upinzani na siyo vingine,” amesema Uhagile.