Dada wa kazi apewe maua yake

Dar es Salaam. Dokta Remmy Ongala aliwahi kuimba wimbo wa kuwasifu madereva wote wa Tanzania. Katika maneno yake, wimbo uliwataja madereva wa Serikali, wa mashirika ya umma, Idara, Wizara na pia madereva wa makampuni.

Humo kuna madereva wa usafiri wa umma kama UDA na KAMATA. Ingelikuwa wimbo huo umetungwa hivi karibuni kwa ninavyomjua Remmy, asingekosa kutaja madereva wa mwendokasi, daladala na bodaboda.

Wimbo huu una tafsiri kubwa kwamba “mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni”. Hata kama mtu anafanya kazi isiyo na kipato kikubwa wala wasifu mrefu lakini ilimradi ni ya halali, anapaswa kuvikwa maua yake kama motisha. Nijuavyo mimi wanamuziki wa sasa ni rahisi zaidi kuwaimba au kuwasifia “mapedeshee”, ambao kila wanapotajwa huenda kulipa fadhila kwa wanamuziki. 

Nakumbuka King Yellowman aliutambulisha wimbo wake maalumu kwa maneno haya “Hiki ni kitu maalumu (spesho rikwest) kwa wanawake wote wafanyao kazi”. Nikamsikiliza na kugundua aliwapa sifa za ujumla bila kuainisha tofauti za kimajukumu za wanawake. 

Kuna wanawake wanaofanya kazi muhimu sana kwa ustawi wa jamii, halafu jamii hiyohiyo haitambui mchango wao kwenye maisha. Wanawake hawa ni madada wa kazi. 

Kusema ukweli dada wa kazi hatofautiani na dereva wa nyumba. Kama ingelikuwa kazi zao zote zinaainishwa kwenye mikataba rasmi, madada hawa wangelipwa fedha nyingi kuliko waajiri wao.

Lakini kinachoonekana mapema ni usafi wa nyumba na mazingira yake, upishi na uangalizi wa watoto tu. Siyo mbaya kudhani hivyo, lakini dada wa kazi anakwenda mbali zaidi kwa kuishika nyumba ibaki kwenye mstari wake bila kuyumba.

Jambo la kwanza, dada wa kazi hufanya majukumu yake kwenye mazingira magumu na hatarishi. Hakuna atakayepinga nikisema asilimia kubwa ya wanawake hutazamana kwa jicho la pembe. Anapoingia ndani ya nyumba tu, mama mwenye mji humkodolea jicho la mtetea dhidi ya kunguru aliye juu ya mti.

Haishangazi kwani wasiwasi ndio akili kunguru anaweza kukwapua kifaranga wakati wowote na kutokomea zake. Hivyo mama inampasa kuchunga mzigo wake.

Jambo lingine ni kwamba haitazamwi huyu dada anatokea pande zipi. Tumezoea kuona watu wanaonuia kufunga ndoa na kuishi pamoja wakidumu kwenye mahusiano kwa muda kwa lengo la kuchunguzana tabia. Wakishakubaliana na madhaifu yao ndipo huoana.

Lakini dada wa kazi anaitwa leo na anatakiwa kuanza kazi leo. Haijalishi anatokea Iringa Vijijini, uchagani wala umakondeni, mapungufu yake yatanyoshwa na mama mwenye nyumba.

Mambo haya ni magumu sana. Nakumbuka katika enzi zetu, mchezaji mmoja wa timu ya Taifa aliyeletwa kutoka Kanda ya Ziwa alisusia mazoezi ya kocha uwanjani. Alikosea kumiliki mpira mara mbili mfululizo, kocha akakasirika na kumtupia maneno makali ya kipwanipwani: “We*@# nini!!! Toa pasi kule…*@# mkubwa we!!!” 

Mchezaji yule alikaribia kumkwida kocha kwa hasira, lakini wenzake wakamzuia. Aliondoka huku machozi yakimlenga.

Ndivyo baadhi ya madada wa kazi wanavyopokea maelekezo kutoka kwa mabosi wao. Huenda mama ameanza kupata kamsongo kutokana na urembo wa mdada huyu, sasa anaweza kufanya lolote kuupunguza 

msongo wake ukizingatia yeye ndiye bosi. Iwapo dada huyu aliletwa kutoka kwa ndugu wa mume basi ujue atakuwa na jukumu la ziada katika kuilinda ndoa hiyo isimeguke.
 Masikini pamoja na kuwa kosa si lake, lakini anaongezewa jukumu bila malipo ya ziada.

Lakini pia iwapo dada yetu ataamua kujibu mapigo ya mama, atahatarisha nyumba kuvunjika bila kutoa nyufa. Kumbuka yeye ndiye mpishi wa chakula chenu cha kila siku; akizingua nyote mtajikuta chali.

Lakini pia yeye ndiye mlezi wa watoto. Sehemu zingine akinamama wanawalazimisha watoto wawapende kwa maneno ya “switiiii… mami is hia…” na vijizawadi vya biskuti. Lakini watoto wanakuwa wamemwelewa sana dada mlezi wao.

Inasemwa kuwa kwenye mafanikio ya mwanaume, mwanamke anahusika kwa ukubwa sana. Wakati mwanaume anapambana kuikidhi familia kwa mahitaji yote muhimu yakiwemo chakula, mavazi, malazi, matibabu, elimu, kodi na kadhalika, mke anapaswa kuchukua majukumu ya ulezi na utunzaji wa familia.

Lakini kwa vile mke naye ana mahangaiko mengine kama ujasiriamali au vikoba, hapa ndipo inapomlazimu kumpata msaidizi kwenye baadhi ya maeneo.

Lakini mara baada ya mdada wa kazi kuingia, mke anasahau majukumu yake yote na kuyabwaga kwa mjakazi. Atarudi saa sita za usiku akute mumewe ameshapikiwa, ameshaoga na kula na sasa ameketi sebuleni akitazama TV. 

Mama naye atajiketisha kando ya mumewe kwenye TV. Mguu ukiwa juu ya stuli, atamuuliza dada kama watoto wameshalala.

Sasa mdada wa kazi atatandika kitanda cha mzee, na atafua hadi nguo zake za ndani. Si ajabu wakati mzee akitoka kwenda kazini, yeye ndiye atakayemrekebisha kona za ukosi wa shati.

Baada ya hapo atawaandaa watoto waende shule, na wakirudi awasimamie kufanya masomo yao ya nyumbani. Hakyanani wanaume tumeumbiwa mateso! Lakini yote kwa yote tuwape maua yao na kuwaombea waendelee hivyo mara wakipata wenza wao.

Related Posts