Morogoro
Kufuatia kero ya muda mrefu ya kutokuwa na kivuko cha uhakika katika mto Mngazi wananchi wa kata za Singisa na Mngazi, wameishukuru serikali kupitia TARURA kwa kuwaondolea kero hiyo kwa kuwajengea daraja la kudumu.
Daraja hilo lenye urefu wa mita 45 katika barabara ya Mngazi- Singisa linaunganisha kata za Mngazi na Singisa katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro mkoani Morogoro.
Bw. Fredrick Paulo Meda ambaye ni Afisa Mtendaji Kata ya Singisa ameishukuru serikali kwa kuwajengea daraja kwani kabla ya ujenzi wa daraja hilo walikuwa wanapata shida hususani kwenye mambo ya kijamii na kiuchumi.
“Kipindi cha masika maji yakijaa kuvuka gharama ilikuwa juu kwani gharama ya uvushaji kwa mtu mmoja ilikuwa shilingi 1000, ukiwa na bodaboda ilikuwa ni kati ya shilingi 3000 na shilingi 4000, mizigo kuanzia kilo 100 na kuendelea ilikuwa shilingi 5000-6000 kwa hiyo kupitia daraja hili linakwenda kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi katika maeneo haya”, amesema.
Naye, Bi. Jennifer Paulo amesema kuwa anashukuru kwa ujenzi wa daraja hilo kwani kabla ya daraja maji yakijaa hususani kwa wazazi kipindi cha kujifungua ilikuwa ni shida kuvuka kwenda upande wa pili iliko hospitali hivyo iliweza kupelekea hata vifo kwa mama na mtoto.
Naye, Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Morogoro, Mhandisi Wilbroad Lemau amesema kuwa mradi huo unaotekelezwa kupitia mradi wa RISE chini ya programu ya kuondoa vikwazo katika barabara umekuja kutatua changamoto za wananchi wa kata za Mngazi, Singisa na Bwakila Juu.
Kwa mujibu wa Mhandisi Lemau, kabla ya ujenzi wa daraja hilo, wananchi wa kata hizo walikuwa wakishindwa kusafirisha kwa urahisi mazao yao ya kilimo hasa karafuu, tangawizi na mizigo mengine.