FBI yapata bosi mpya mwenye asili ya Tanzania, asimulia mateso ya Iddi Amin

Mkurugenzi mpya wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), Kash Patel ameelezea undani wa asili yake kuwa ni Afrika Mashariki, huku akitaja sababu ya familia yake kuhamia Marekani.

Patel aliyezaliwa Februari 25, 1980 amesema mama yake ni Mtanzania, baba yake alizaliwa Uganda lakini walilazimika kuhama mwaka 1972 baada ya amri ya aliyekuwa Rais wa Uganda, Idd Amin.

Hayo ameyasema jana Februari 21, 2025 wakati wa uapisho wake.

Patel amesema familia yake ililazimika kukimbia nchini Uganda mwaka wa 1972 wakati Idi Amin alipoamuru kufukuzwa kwa jumuiya ya Waasia, tukio ambalo lilisababisha watu wengi kuhama makazi yao na kuyumba kiuchumi huku wengi wakikimbilia Uingereza, Canada, na Marekani.

“Rais Donald Trump aliponifahamisha nia yake ya kuniteua kuwa mkurugenzi wa FBI, nikaona kuwa sibebi ndoto za wazazi wangu tu, bali pia matumaini ya mamilioni ya Wamarekani wanaosimamia haki, uadilifu na utawala wa sheria.

“Baba yangu alikimbia udikteta na mauaji ya halaiki nchini Uganda enzi za Idd Amin ambapo wanaume, wanawake, na watoto 300,000 waliuawa kutokana na asili zao, kwa sababu tu walifanana na mimi (Waasia). Mama yangu anatokea Tanzania, alisoma India, kama vile baba yangu, na walifunga ndoa huko,” anasimulia Patel.

Patel anasema baada ya mauaji hayo na jamii ya Waasia kufukuzwa Uganda, wazazi wake walihamia (Baba na mama yake) walihamia Marekani.

“Baadaye walihamia New York, ndiko nilikozaliwa kama seneta alivyosema,”amesema Patel.

Patel amesema maadili aliyopewa katika ukuaji wake yamekuwa na nguvu ya kuendesha kazi yake katika miaka 16 ya utumishi wa serikali.

“Kulinda haki za katiba ni jambo la muhimu sana kwangu na imekuwa kila mara nilipokula kiapo hicho,”amesema.

Safari yake katika ujasusi

Alifahamika zaidi alipokuwa kama mwanasheria mkuu wa Kamati ya Ujasusi ya Bunge, ambapo alichukua jukumu muhimu katika uchunguzi wa kuingiliwa kwa Russia katika uchaguzi wa Marekani.

Baadaye, kama mshauri mkuu wa Rais Donald Trump katika muhula wake wa kwanza, alijulikana kwa ukosoaji wake wa jumuiya ya kijasusi na urasimu wa shirikisho.

Kitabu chake Government Gangsters kilieleza kwa kina imani yake kwamba mfumo wa haki wa Marekani ulikuwa umeingiliwa na upendeleo.

Licha ya kukabiliwa na ukosoaji kwa maoni yake, Patel amebaki imara katika kujitolea kwake kurekebisha taasisi za kutekeleza sheria.

Related Posts