MASHABIKI wa Yanga wana kiu ya kumwona nyota mpya wa timu hiyo, Jonathan Ikangalombo ‘Ikanga Speed’ aliyesajiliwa dirisha dogo kutoka AS Vita ya DR Congo akiliamsha katika kikosi hicho, lakini siku zimepita bila winga huyo kuonekana na kuzua maswali.
Hata hivyo, kocha mkuu wa kikosi hicho, Hamdi Miloud ameamua kukata mzizi wa fitina kwa kuanika kila kitu kuhusu nyota huyo Mkongamani wakati kikosi hicho kikiwa kimetua Kigoma kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa itakayopigwa Jumapili.
Yanga itakuwa wageni wa Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma na Kocha Miloud Hamdi ameondoka na mchezaji huyo katika msafara wa timu hiyo kwa ajili ya mchezo huo, huku akiweka wazi jamaa yupo tayari kukiwasha kwani kila kitu kwake sasa kipo freshi.
Winga huyo anayemudu kucheza pia kama mshambuliaji wa mwisho, alitua Jangwani wakati wa kocha Sead Ramovic, lakini tangu atue dirisha dogo hajawahi kucheza mechi hata moja, huku kocha aliyeondoka akisema, alikuwa na uzito na mwili mkubwa jambo lilimfanya akae nje kwa mazoezi zaidi.
Hadi Ramovic anaondoka Yanga, Ikanga Speed aliishia kufanya mazoezi tu, huku suala la kucheza katika mechi za Ligi Kuu na hata ile ya Kombe la Shirikisho (FA) akisikia kwenye bomba tu, kwani hata Hamdi alipoajiriwa kutoka Singida BS akiiongoza Yanga katika mechi tatu jamaa ameishia jukwaani tu.
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti, Hamdi alisema Ikanga ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na anataka kuanza kumpa muda wa kucheza, kwani anamwona yuko sawa na hana uzito kama awali.
“Kuhusu ishu ya uzito wa mwili niliikuta hiyo taarifa, lakini kwa sasa sioni kisingizio hicho tena na ameonyesha kitu kikubwa mazoezini,” alisema Hamdi na kuongeza;
“Ikanga ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na ninataka kuanza kumpa muda wa kucheza, nimemuangalia kwa kipindi hiki kifupi namuona ni winga mzuri akipewa nafasi.”
Tangu dirisha dogo kufungwa hadi sasa Yanga imecheza jumla ya mechi tano huku ikishinda nne na kutoka suluhu moja dhidi ya JKT Tanzania na kesho Jumapili itavaana na Mashujaa ambao katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam iliifunga mabao 3-2 kwenye Uwanja wa KMC Complex.