Kilichomkwamisha Morrison KenGold hiki hapa

WAKATI mashabiki wa KenGold wakisubiri kwa hamu kumuona uwanjani staa mpya wa timu hiyo, Bernard Morrison, nyota huyo bado ataendelea kuwa nje ya uwanja hadi taratibu za vibali vya kazi nchini vitakapokamilika.

Morrison aliyewahi kutamba na timu za Yanga na Simba kwa misimu tofauti, alisajiliwa na KenGold dirisha dogo lililofungwa Januari 15 akiwa huru, ambapo hadi sasa hajacheza mechi yoyote kati ya tano zilizochezwa mzunguko wa pili.

Staa huyo asiyeishiwa na vituko ndani na nje ya uwanja, alitambilishwa nchini msimu wa 2019/20 akiitumikia Yanga, ambapo alicheza mechi 13 akifunga mabao manne na asisti tatu, ambapo msimu uliofuata alijiunga na Simba.

Hata hivyo, kabla ya kutua kwa Wekundu, nyota huyo alikumbana na mgogoro baina yake na Yanga ambapo kesi yake ilifika Mahakama ya Usuluhishi ya Kesi za Michezo Duniani (Cas) ambako aliwabwaga mabosi hao wa Jangwani.

Akiwa na Wekundu msimu wa 2020/21, nyota huyo alicheza mechi 24 akifunga mabao manne na kuhusika kwenye mengine sita kabla ya kuachwa uliofuata na kuwa huru akaibukia FAR Rabat ya Morocco alikodumu msimu mmoja ndipo akanaswa na KenGold  dirisha dogo msimu huu.

Mwanaspoti limeshuhudia nyota huyo akipewa programu maalumu za kujifua mwenyewe na muda mwingine akiungana na wenzake katika mazoezi ya pamoja huku ikielezwa kuwa hajawa tayari kutumika.

Awali, taarifa za ndani zilieleza kuwa staa huyo raia wa Ghana anakabiliwa na majeraha, lakini habari za kuaminika ni kwamba kiungo huyo amepewa mazoezi maalumu huku benchi la ufundi likimuangalia ubora wake.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Benson Mkocha ameliambia Mwanaspoti kuwa kutoonekana uwanjani Morrison ni kutokana na vibali kutokuwa tayari akieleza kuwa matarajio ni baada ya mechi dhidi ya JKT Tanzania.

Kuhusu ishu ya kocha wa timu hiyo Mserbia Vladslav Heric, Mkocha alisema vibali vyake vimekamilika, japokuwa hatakuwa mkuu kutokana na kukosa sifa kwa kuwa hajafanya kozi ya ‘riflesha’ ili kumthibitisha katika nafasi hiyo.

“Morrison kibali cha kazi bado, hakuna changamoto nyingine zaidi na tunatarajia baada ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania anaweza kuonekana uwanjani. Uongozi unapambana kukamilisha hilo haraka na mapema,” alisema Mkocha.

“Kocha vibali vimekamilika ila hajapata ‘riflesha kozi’ kumthibitisha kukaa benchi kama kocha mkuu. Kimsingi tunapambania matokeo mazuri kila mechi ili kuwa nafasi nzuri” alisema Katibu huyo.

Related Posts