Kwa nini wazazi wawe kikwazo cha mtoto kuoa, kuolewa

Dar es Salaam. Vuta picha umekwenda kumtambulisha mchumba unayetarajia kumuoa wazazi wakamkataa, wa pili pia, hali hiyo ikajirudia kwa wa tatu.

Kuwakataa ni jambo moja, sababu wanazotoa kuhusu uamuzi huo ni jambo jingine. Wa kwanza, wamemkataa kwa sababu haendani nawe.

Mchumba wa pili wamedai hastahili kuwa mke kwa kuwa ana historia ya kupata malezi ya mzazi mmoja (single mother), lakini wa tatu, kwa sababu asili yao.

Unaweza kudhani ni hadithi … Huu ni uhalisia wa maisha anayopitia kijana Adam Eden (si jina halisi) anayefikisha miaka 39 mwaka huu, mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Eden, licha ya kupeleka wachumba watatu kuwatambulisha kwa wazazi wake, wote wamekataliwa kwa sababu anazoeleza haoni kama zina mashiko.

Kijana huo anayemiliki duka la nguo eneo la Kariakoo anasema kila mchumba aliyempeleka kwa wazazi wake alivaa inavyompasa mwanamke anayekwenda kutambulishwa ukweni, bado hapati jawabu kwa nini wakataliwe.

Kila anapowauliza wazazi wake, anaeleza wanamtajia sababu bila maelezo ya kina kiasi kwamba amefikia uamuzi wa kumtafuta mwenza atakayeishi naye bila kuwashirikisha wazazi.

“Fikiria unamchukua mtoto wa mtu unakwenda kumtambulisha anakataliwa, unamuacha mwingine vivyo hivyo, nitamuoa nani sasa. Wazazi hawanipi sababu zenye mashiko, hadi sasa sielewi wanataka mwanamke wa namna gani,” anasema.

Eden anasema amewahi kuzungumza na wazazi wake wamweleze kuhusu mwanamke wanayemhitaji lakini hakupata majibu ya kina.

“Wananiambia awe na upendo kwangu, wakati niliowapeleka wote wananipenda. Wananiambia awe mwenye heshima kwangu na kwao, wakati niliowapeleka waliniheshimu sana,” anaeleza.

Uamuzi wa Eden kutafuta mchumba nje ya Dar es Salaam na kwenda kumtambulisha kwa wazazi wake anasema ulitokana na kukataliwa kwa wawili wanaoishi Dar es Salaam.

Hata hivyo, huyo alikataliwa kwa kigezo cha asili yake kuwa mbali na jiji hilo.

Kijana huyo ambaye wazazi wake wana asili ya Mkoa wa Iringa na wacha Mungu, anasema wachumba aliowapeleka walikuwa wa madhehebu sawa na ya wazazi wake.

Anasimulia anayoyapitia yeye kutoka kwa wazazi wake ni tofauti na ilivyokuwa kwa dada na kaka yake, ambao hawakupata vikwazo na wanaendelea na maisha na wenza wao.

“Nafikiri niwe na mwanamke bila wazazi kujua tuishi maisha yetu, tuzae watoto hata wawili kisha niwapelekee wajukuu, naamini hawatawakataa. Hata wasipomtaka mkwe wajukuu watawapokea,” anaeleza.

Si kijana huyo pekee aliyekumbwa na mkasa huo, Joan Mussa (si jina halisi) amejikuta akikataliwa na wazazi wa wanaume wawili waliokwenda kumtambulisha.

Anasema alikataliwa kwa sababu ya kabila lake, wazazi wa mwanamume wanaotokea Mkoa wa Tanga, walidai mtoto wao hawezi kuoa Msukuma.

Anasema kwa mwanamume mwingine aliyekuwa Mnyakyusa, wazazi wake walimkataa pia.

Kwa sababu ya kumbukumbu hizo, anaeleza alipopata mwanamume wa tatu aliyekuwa tayari kwenda kumtambulisha, alimweleza mapema kwamba alishakataliwa na wazazi wa wanaume wawili.

“Nikamwambia kama anataka kunioa tufanye kitu kitakachosababisha nisiumizwe tena, ikabidi nibebe ujauzito. Nimekwenda kutambulishwa nikiwa mjamzito,” anasema.

Awali, anasema wazazi wa mwanamume walimkataa, lakini walikubali aolewe baada ya mumewe kuwaeleza kuwa alikuwa mimba.

“Mwanamume akawaambia wazazi wake kuwa nimebeba mimba yake, ikabidi wazazi wakubali kwa shingo upande, nikaolewa hadi sasa miaka mitano imepita tunaishi na mume wangu,” anaeleza.

Kwa upande wake, Aneth Langa (si jina halisi) anaeleza alikataliwa ukweni licha ya kuwa mjamzito.

“Wazazi wake wakasema watashirikiana na mtoto wao kulea mimba hadi mtoto lakini siyo niolewe. Ilibidi iwe hivyo hadi sasa,” anasema.

Kuna umuhimu wa wazazi kumpa mtoto uhuru wa kuamua aina ya mwenza anayemhitaji, waepuke kuwa kikwazo, kama inavyoelezwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania, Antonia Sangali.

Chifu Sangali anasema kwa sababu mtoto ndiye atakakwenda kuishi na huyo mwenza, hakuna sababu ya mzazi kuingilia.

Anasema kitendo cha mzazi kuingilia uamuzi wa mtoto kuhusu mahusiano ya mapenzi, kinasababisha msongo wa mawazo na hatimaye matukio ya kujiua.

“Mtoto akileta mchumba, unapaswa kumpokea usiwe kikwazo kwa sababu ndoa ni suala la makubaliano ya wawili na mapenzi yao,” anasema.

Anasema vikwazo vinavyosababishwa na wazazi kuhusu ndoa za watoto huwasababishia msongo wa mawazo na hatimaye kuharibikiwa.

“Watoto tusiwaingilie, sisi tupokee. Haya mambo mengine tunayoyafanya si ya kwetu, tuwaache watoto wawe huru kuamua,” anasisitiza.

Anasema ulikuwepo wakati wa wazazi kuwatafutia watoto wenza, lakini si sasa kwa sababu wana maeneo mengi ya kukutana na wachumba kuliko zamani.

“Zamani mtoto hakuwa anatoka nyumbani mara kwa mara na hakuwa na safari nyingi, lakini sasa mtoto anakwenda kusoma chuoni hakai na wewe miaka kadhaa, huko anakutana na mchumba akikuletea mpokee,” anaeleza.

Anasema hayo ni miongoni mwa mambo ambayo machifu wanayashughulikia hivi sasa, kwa sababu maisha yamebadilika hata mitazamo ya wazazi inapaswa ibadilike.

Kwa mtazamo wa mwanazuoni wa saikolojia, Dk Chris Mauki, yanayotokea kwa wachumba kukataliwa yanachochewa na tatizo kutoka kwa wazazi na siyo wanawake waliopelekwa kutambulishwa.

Dk Mauki anasema tatizo linatokana na wazazi kuwa na matakwa yao na kwa sababu hiyo, wanataka kumuolea mtoto wao, badala ya kumpa nafasi aoe.

“Katika hali kama hiyo, inaonyesha wazi kuwa wazazi wana matakwa yao na hilo ndilo kosa kubwa la wazazi wengi. Hawapaswi kumuolea mtoto bali anapaswa kuachwa aamue na wamwezeshe afanikishe,” anaeleza.

Anasema kwa yaliyomfika Eden ikitokea ameoa, inaonekana wazi wazazi wake wataingilia maisha ya ndoa yake.

“Hata huyo muoaji ikitokea amefanikiwa kuoa, ndoa yake ikidumu kwa miaka mitano, nitafute tena tufanye mahojiano,” anaeleza Dk Mauki.

Mwanazuoni wa Sosholojia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Lacius Mugisha anasema kabla ya kuoa, kijana anapaswa kuwa na mawasiliano mazuri na wazazi wake.

Mawasiliano hayo kwa mujibu wa Dk Mugisha, yatawezesha kuwaaminisha wazazi tabia za mtu unayetaka kumuoa au kuolewa naye kwa sababu wewe ndiye uliyemwona kwa muda mrefu zaidi yao.

Anasema mawasiliano pia yana nguvu katika kujenga ushawishi kwa wazazi ili wamkubali mchumba utakayempeleka, kinyume cha hayo kuna uwezekano wa kukwama.

Anasema wapo wazazi wenye matarajio makubwa yasiyo na uhalisia kuhusu mchumba anayefaa ikiwamo kabila, dini, hadhi ya kifamilia au hali ya kiuchumi.

Wengine anasema hutumia ushawishi mkubwa kwa hofu ya kupoteza mamlaka juu ya maisha ya kijana wao, hivyo kumnyima uhuru wa kuchagua mweza.

“Baadhi ya familia wazazi wanakuwa vikwazo vya ndoa za vijana wao na unafika wakati wanawatishia ili kumshurutisha aendane na kile wanachokitaka,” anasema.

Anasema utegemezi pia ni sababu nyingine inayowafanya baadhi ya wazazi wasitamani vijana wao wasioe au kuolewa wakidhani watakosa msaada aliokuwa akiwapa kabla ya kuwa kwenye ndoa.

Kwa mtazamo wa kiimani, Padri Clement Kihiyo wa Kanisa Katoliki anasema wakati wa kupeleka mchumba kwa wazazi, umri ni kigezo cha kwanza unachopaswa kuzingatia.

Anaeleza sheria za Tanzania zinataka mwolewaji au muoaji awe na umri wa zaidi ya miaka 18, chini ya hapo hata wazazi kama wanaelewa hawawezi kuruhusu.

Anasema mwonekano alionao anayekwenda kutambulishwa siku ya utambulisho ni jambo linaloamua wazazi wamkatae au kumkubali.

“Wazazi mara nyingi wanaangalia maadili kwa wanayepelekewa kutambulishwa, akivaa isivyompasa, wazazi watamtafsiri kuwa hana maadili na inakuwa vigumu kumkubali,” anasema.

Anaeleza wakati mwingine wazazi wanauliza kutaka kujua mlikofahamiana, kwa muda gani na wangependa wasikie habari njema kuhusu kijana au binti husika.

“Wakiona unajikanyaga kanyaga unashindwa kumuelezea uliyekwenda kumtambulisha vema, hili ni wazi kabisa hawatamkubali kwa sababu watajua humjui,” amesema.

Padri Kihiyo anasema hata taratibu za dini ya Kikristo zinataka maadili ya kidini na kijamii kwa muoaji na muolewaji.

Imamu wa Msikiti wa Tununguo mkoani Morogoro, Sheikh Seif Khatibu anasema kwa imani ya dini ya Kiislamu hakuna utamaduni wa wenza kwenda kutambulishana kwa wazazi kabla ya kuoana.

Kinachofanyika anasema kijana humtuma mwakilishi katika familia anayotaka kuoa ili akaeleze nia yake na anayetumwa anapaswa kuwa mwenye busara na maadili.

“Kwa sababu anayetumwa ndiye anayewakilisha familia ya muoaji, akionyesha tabia mbaya hatapokewa,” anasema.

Related Posts