Kwa Simba hii, ukijichanganya inakula kwako!

KUWENI makini! Ndivyo unavyoweza kusema kwa timu pinzani pale zinaposhuka uwanjani kucheza na Simba, kwani zikijichanganya kidogo tu zijue mapema inakula kwao mapema.

Ndio, Simba inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na inayousaka ubingwa wa ligi hiyo baada ya kuukosa kwa misimu mitatu mfululizo, msimu huu imekuja kivingine kiasi inashtua kwa namba ilizonazo hadi sasa.

Kama hujui ni kwamba miamba hiyo imesababisha wapinzani kupata kadi nyekundu tatu, lakini ikivunna jumla ya penalti 10 hadi sasa na tisa kati ya hizo ikiinufaisha timu hiyo kwani imepoteza moja tu. Namba hizo zinatoa picha kwamba ni lazima timu yoyote inayocheza na Simba inapaswa kuwa makini kwenye eneo la lango lao kwa kutoruhusu nyota wa Wekundu hao kuingia ndanio ya boski au kukabiliana nao bila kutumia akili kubwa, la sivyo zitaendelea kuumia mbele yao.

Hata hivyo, Simba haipo pekee yake kwa timu ilizoponza wapinzani, kwani Pamba Jiji nayo imeponza timu tatu ilizocheza nazo zikilimwa kadi nyekundu kama ilivyofanya Simba hadi sasa wakati zikiwa zimeshatolewa kadi nyekundu 18 kama ilivyo msimu uliopita.

Kadi nyekundu ya juzi ya Mrundi Derrick Mukombozi wa Namungo aliyoipata, imeifanya kufikisha tatu za Simba msimu huu, ambayo ilizua sintofahamu kubwa kutokana na kutoeleweka kosa gani alilolifanya nyota huyo na kusababisha kutolewa nje.

Katika mchezo huo, ilishuhudiwa penalti tatu zikitolewa na mbili kati ya hizo zilizopigwa zilizama wavuni ambazo ni za kiungo, Jean Charles Ahoua huku moja ya mshambuliaji, Leonel Ateba ikidakwa na kipa wa Namungo, Jonathan Nahimana.

Kadi nyingine nyekundu iliyotolewa mchezo wa Simba, ni ya kipa wa Fountain Gate, John Noble wakati timu hizo zilipotoka sare ya kufungana bao 1-1, kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Manyara Februari 6, mwaka huu.

Nyingine ilikuwa ya nyota wa maafande wa JKT Tanzania, Mohamed Bakari Desemba 24, mwaka jana Uwanja wa KMC Complex na kikosi hicho kilishinda bao 1-0, la Jean Charles Ahoua kwa penalti.

Kwa upande wa Pamba iliziponza Azam FC kwa aliyekuwa beki wake wa kushoto Cheikh Sidibe kuwa nyota wa kwanza msimu huu kulimwa kadi hiyo zilipokutana Azam Complex, Chamazi kisha Foutain Gate wakati Abalkassim Suleiman aliyepo Pamba kwa sasa kulimwa kadi na Ramadhani Chabwedo wa KenGold naye aliingia 18 za Wanakawekamo timu hizo zilipokutana.

Kwa upande wa Yanga katika michezo miwili wapinzani walilimwa kadi nyekundu akianza Saleh Masoud wa Pamba Jiji kikosi hicho cha Jangwani kikishinda 4-0, Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Oktoba 3, mwaka jana.

Kisha kipa wa JKT Tanzania, Denis Richard aliyoipata wakati timu hiyo ya maafande ilipochapwa 2-0, yaliyofungwa na Pacome Zouzoua na Clatous Chama katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex Oktoba 22, mwaka jana. Nyota anayeongozwa kwa kulimwa kadi nyingi ni Abalkassim aliyepewa mbili, moja akiwa Fountain Gate na nyingine Pamba.

Kijumla hadi sasa zimetoka jumla ya kadi nyekundu 18 kama ilivyokuwa msimu mzima uliopita, huku Simba ikionekana tishio zaidi kwani imenufaika pia kwa timu hiyo kupata penalti 10, ikizifunga tisa zikifungwa na moja ikipotezwa wakiwa ndio kinara.

Penalti za Simba zimefungwa na Jean Charles Ahoua aliyefunga tano akiwa ndiye kinara kwa sasa, huku nyingine nne zikiwekwa kimiani na Leonel Ateba kati ya tano alizopiga akilingana na Stephane Aziz Ki wa Yanga anayeongoza kwa kupiga penalti nyingi (sita) hadi sasa, akipoteza mbili.

Kijumla Simba imepiga penalti 10 kati ya 58 zilizopigwa katika ligi hiyo (kabla ya mechi za jana), ikiwa ndio kinara ikifuatiwa na Yanga iliyopiga saba na kupoteza mbili

KenGold, KMC na Fountain Gate ndio timu iliyosababisha na kupigiwa penalti nyingi (7) zikifuatiwa na Namungo (sita), huku jumla ya penalti 12 kati ya 58 zilizopigwa hadi sasa zimekoswa (kabla ya mechi za jana), hali inayoonyesha hadi ligi itakapotamatika Mei 25, kunaweza kushuhudiwa kadi nyekundu na penalti zaidi kutokana na ushindani uliopo katika ligi hiyo na namna waamuzi wanavyojichanganya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Abalkassim anayeongoza kwa kulimwa kadi nyingi nyekundu, alisema suala la kuonyeshwa kadi nyekundu huwa linatokea tu kwa bahati mbaya na sio kama mchezaji anakusudia.

“Tangu nimeanza kucheza soka la ushindani nilikuwa sijawahi kuonyeshwa kadi nyekundu ila msimu huu mambo yamekuwa ni magumu kwangu, nikiri wazi naendelea kujifunza na kukua kutokana na changamoto mbalimbali zinazotokea maishani mwangu.”

Abalkassim alianza kulimwa kadi dhidi ya Fountain Gate katika mchezo wa kikosi hicho dhidi ya Pamba Novemba 5, mwaka jana na juzi kati tena akiwa na Pamba aliyojiunga nayo dirisha dogo akitokea Fountain Gate, alipata dakika ya 62 ya mchezo na kushuhudia kikosi hicho cha jijini Mwanza kikichapwa mabao 2-0, mbele ya Mashujaa FC.

Nyota wengine waliopata kadi nyekundu ni Cheikh Sidibe (Azam FC), Saleh Masoud (Pamba Jiji FC), Victor Sochima (Tabora United), Ibrahim Elias (KMC FC), Denis Richard (JKT TZ), Ibrahim Hamad ‘Bacca’ (Yanga) na Abalkassim Suleiman (Fountain Gate), Joseph Mahundi (Kagera Sugar), Masoud Issa ‘Cabaye’ (KenGold).

Wengine ni Ramadhan Chobwedo, Zawadi Mauya (KenGold), Meshack Abraham (TZ Prisons), Mohamed Bakari (JKT TZ), Eric Okutu (Pamba Jiji FC), John Noble (Fountain Gate), Ismail Mpank (KMC FC), Abalkassim Suleiman (Pamba FC) na Derrick Mukombozi (Namungo FC).

Related Posts