Shinyanga. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amembana mkandarasi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa uwanja huo ifikapo Aprili 2025, kama alivyoelekeza Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa.
Februari 19, 2025, Waziri Mkuu alitua katika uwanja huo na kubaini kwamba haukuwa na taa, hivyo aliagiza kufikia Aprili 2025, mkandarasi ahakikishe ndege zinatua usiku katika uwanja huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 74 huku eneo la kutua ndege (runway) likiwa limekamilika.
Jaja, Februari 21, 2025, Waziri Mbarawa alitembelea uwanja huo na kuhoji kuhusu mchakato wa ununuzi wa taa huku akihimiza kukamilishwa kwa ujenzi wa uwanja huo kwa wakati ifikapo Aprili 2025.
Akizungumza kwenye ziara yake hiyo, Waziri Mbarawa amehimiza ununuzi wa vifaa vya uwanja huo kutoka kiwandani na kwamba ufanyike haraka ili uwanja huo utumike muda wote wa mchana na usiku.
“Waziri Mkuu amesema anataka kutua usiku katika uwanja huu usiku, je, mmeagiza vifaa kama taa za kuongozea ndege na kiwango cha juu cha ardhi (AGL)? Sababu vifaa hivi vinahitaji uagizaji maalumu kutoka kiwandani na inahitaji muda, kama hamjatoa maagizo lazima tupambane agizo lifanyike sasa hivi,” amesema Mbarawa.
Waziri Mbarawa ameongeza kuwa ujenzi wa uwanja huo umegharimu Sh52 bilioni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kwamba utasaidia viwanja vikubwa vya Mwanza na Dar es Salaam, ndiyo maana zinatua ndege ndogo.
“Viwanja vya ndege vya mikoa kama Shinyanga, Tabora, Kahama na Musoma, hivi tunaviita Feeder Airports ambavyo vinasaidia viwanja vikubwa kama Mwanza na Dar es Salaam, ndiyo maana zinatua ndege ndogo kama Bomberdier Q400. Uwanja huu utagharimu Sh52 bilioni hadi kukamilika kwake pamoja na VAT,” amesema Mbarawa.
Mhandisi mshauri wa ujenzi huo kutoka Airport Shinyanga, Sostenes Lweikiza amesema kuwa sehemu ya vifaa vimeagizwa japo siyo vyote lakini bado hajapata asilimia ngapi ya vifaa imeagizwa gharama kiasi gani imetumika.
“Sehemu ya vifaa hivyo imeagizwa lakini bado hatujapata taarifa kutoka kwa muagizaji ni asilimia ngapi ya vifaa iliyoagizwa lakini baada ya kufika tutakuwa na ripoti kamili,” amesema Lweikiza.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amesema kuwa uwanja huu ni suluhisho kwa wafanyabiashara wa madini kwa safari za anga pia utahudumia baadhi ya mikoa ya jirani na suala la uhamishaji wa makaburi unafanyika kwa utaratibu na uwanja utakuwa huru.
“Uwanja huu utarahisisha safari za anga kwa wafanyabiashara wa madini na pia utahudumia mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Tabora baadhi ya wilaya zinazopakana na Shinyanga pia uhamishaji wa makaburi katika uwanja huu unafanyika kwa kufuata mila na desturi za eneo husika baada ya hapo uwanja utakuwa huru,” amesema Macha.
Msimamizi wa ujenzi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Donatusi Binamungu amesema kuwa mradi huo ulisainiwa mwaka 2017 na kuanza kazi 2023 na unategemewa kumalizika Aprili Mosi, 2025.
“Uwanja huu una mita 2200 ambao unaweza kupokea ndege aina ya Bomberdier Q400 urefu wa uwanja ni kilomita 2.2 na upana wake ni mita 30 na hadi sasa umekamilika kwa asilimia 74 huku njia ya kutua na kuruka (Runway) imekamilika kwa asilimia 100,” amesema Binamungu.