KOCHA wa Tabora United, Mkongomani Anicet Kiazayidi amesema ana kazi kubwa ya kufanya katika michezo ya mzunguko huu wa pili, baada ya kutoka sare ya bao 1-1, ugenini juzi dhidi ya Tanzania Prisons na kufikisha dakika 270 bila ya ushindi.
Kauli ya kocha huyo inajiri baada ya timu hiyo kufikisha sare ya tatu mfululizo tangu mara ya mwisho ilipoifunga Kagera Sugar mabao 2-1 Februari 11, ikianza na 1-1 dhidi ya KenGold, suluhu na Fountain Gate kisha 1-1 na Tanzania Prisons.
“Mzunguko wa pili umekuwa mgumu kwa sababu tumeona timu nyingi zimefanya usajili mkubwa wa wachezaji wazuri. Baadhi yao hapa ni wapya na wanahitaji muda kidogo kuzoeana na waliopo, ingawa mwenendo wao hadi sasa sio mbaya kikosini,” alisema.
Anicet alisema maendeleo ya kikosi chake sio mabaya licha ya kuanza raundi ya pili kwa ugumu, huku akiwataka nyota wa timu hiyo kupambana kuendelea kuonyesha ushindani ili watimize malengo ya kumaliza wakiwa nafasi nne za juu.
Kocha huyo aliyezifundisha AS Vita, Simba Kolwezi, Les Aigles du Congo na Maniema Union za kwao DR Congo, tangu ajiunge na kikosi hicho Novemba 2, mwaka jana amepoteza mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara aliochapwa na Simba kwa mabao 3-0.
Kocha huyo tangu ajiunge na timu hiyo akichukua nafasi ya Francis Kimanzi aliyetimuliwa Oktoba 21, mwaka jana kutokana na mwenendo mbaya ameiongoza Tabora United katika michezo 12, ambapo imeshinda sita, sare mitano na kuchapwa mmoja.
Katika michezo hiyo Tabora ilizifunga Mashujaa bao 1-0, ikaifunga Yanga mabao 3-1, ikashinda 2-0 mbele ya KMC, 2-1 dhidi ya Azam FC, ikaichapa Namungo FC 2-1, kisha ikaifunga Kagera Sugar 2-1 ugenini Februari 11, mwaka huu.
Michezo mitano ya sare ni dhidi ya Singida Black Stars mabao 2-2, (1-1) dhidi ya Coastal Union, (1-1) na KenGold, (0-0) dhidi ya Fountain Gate na (1-1) dhidi ya TZ Prisons, huku kichapo pekee ni cha mabao 3-0 dhidi ya Simba nyumbani Februari 2, mwaka huu.
Katika mchezo huo, Prisons ilianza kupata bao kupitia kwa beki wa kati, Emmanuel Chigozie aliyejifunga dakika ya 67 akiwa katika harakati za kuokoa mpira, huku lile la Tabora likifungwa na mshambuliaji Emmanuel Mwanengo dakika ya 82.
KUU TANGU NOVEMBA 2, 2024
Tabora United 1-0 Mashujaa FC (Novemba 4, 2024)
Yanga 1-3 Tabora United (Novemba 7, 2024)
Tabora United 2-2 Singida BS (Novemba 25, 2024)
KMC 0-2 Tabora United (Novemba 29, 2024)
Tabora United 2-1 Azam FC (Desemba 13, 2024)
Tabora United 1-1 Coastal Union (Desemba 17, 2024)
Tabora United 0-3 Simba (Februari 2, 2025)
Tabora United 2-1 Namungo FC (Februari 5, 2025)
Kagera Sugar 1-2 Tabora United (Februari 11, 2025)
Tabora United 1-1 KenGold (Februari 14, 2025)
Fountain Gate 0-0 Tabora United (Februari 17, 2025)
TZ Prisons 1-1 Tabora United (Februari 21, 2025)