Mtama. Migogoro 27 kati ya 32 ya ardhi iliyowasilishwa katika Kliniki ya Msaada wa Kisheria katika Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi imetatuliwa, huku mitano ikipelekwa katika mamlaka husika.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Rockus Komba, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mnolela, Februari 21, 2025.
Komba amesema wamefanya mikutano katika vijiji sita na kutatua migogoro 27, ikiwemo ya ardhi na ya kifamilia.
“Hadi sasa tumeshatatua migogoro 27 kati ya 32, na iliyobakia tumeshaipeleka sehemu husika ili kupata ufumbuzi. Naamini hadi tutakapomaliza kampeni hii, tutakuwa tumemaliza migogoro yote ya Halmashauri ya Mtama,” amesema Wakili Komba.
Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Lindi, Joyce Kitesho, amewataka wanawake wasifumbie macho ukatili wa aina yoyote ambao unaweza kuhatarisha maisha yao.
“Wanawake wenzangu, nawaomba msifumbie macho masuala ya unyanyasaji majumbani kwetu. Tutoe taarifa, tusifumbie macho,” amesema Kitesho alipokuwa anatoa elimu ya unyanyasaji wa kijinsia na migogoro ya ndoa.
Katika hatua nyingine, wananchi wa Mnolela wameishukuru Serikali kwa kuwaletea msaada wa kisheria katika maeneo yao, wakisema utasaidia kuondoa migogoro mingi inayotokea kwenye jamii zao.
Zabibu Saidi, mkazi wa Mnolela, amesema kampeni hiyo itasaidia kuondoa changamoto za migogoro katika maeneo yao na kuleta suluhu katika jamii.
“Kampeni itatusaidia sisi wananchi wa Lindi kupunguza migogoro inayotokea kila wakati kwenye maeneo yetu, kama migogoro ya ndoa. Nimefurahi sana kuona ipo kwenye orodha kwani wanandoa wengi wananyanyasika majumbani,” amesema Zabibu.