Vatican imesema hali ya kiafya ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis anayeendelea na matibabu hospitali, inaendelea vizuri.
Msemaji wa Vatican, Matteo Bruni amenukuliwa akisema maendeleo ya jumla ya Papa Francis yanaendelea vizuri ambapo Alhamisi asubuhi alikuwa na uwezo wa kutembea mwenyewe akisindikizwa na wasaidizi wake.
Juzi Jumatano, maafisa wa Vatican walieleza kuwa kiongozi huyo aligundulika kuwa na nimonia kwenye mapafu yake yote mawili, jambo litakalochelewesha uponaji wake.
Papa Francis, mwenye umri wa miaka 88, alilazwa hospitalini Ijumaa iliyopita baada ya kubainika kuwa na matatizo katika mfumo wake wa kupumua, ugonjwa ambao kitaalamu huitwa Bronchitis.
Jumapili iliyopita, alishindwa kuendesha misa ya Jumapili Vatican kama ilivyo kawaida kwa kuwa bado alikuwa amelazwa, ambapo maelfu ya waumini wa kanisa hilo kubwa duniani waliungana kumuombea apone haraka.
Jumatatu, madaktari walitoa ripoti nyingine wakieleza kwamba alibainika kuwa na maambukizi mchanganyiko kwenye mfumo wake wa upumuaji.
Ilipofika Jumanne usiku, taarifa ilitolewa kwamba amegundulika kuwa na nimonia kwenye mapafu yake yote mawili, taarifa ambayo iliamsha taharuki miongoni mwa waumini wa kanisa hilo.
Mishumaa na picha nyingi za Papa Francis zimewekwa kwenye sanamu ya Papa John Paul II nje ya Hospitali ya Agostino Gemelli Polyclinic jijini Rome, ambako Papa Francis amelazwa, ambapo waumini wengi wameendelea kumuombea apate ahueni.