Polisi yasema aliyekamatwa kwa nguvu Kibaha alikaidi amri

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema video inayosambaa ikimuonesha dereva bodaboda akikamatwa kwa nguvu katika eneo la Maili Moja, Kibaha mkoani Pwani ni askari walikuwa wanamkamata mhalifu ambaye alikaidi.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Februari 22, 2025 katika kurasa zao za mitandao ya kijamii zimesema kuwa kijana huyo anatuhumiwa kufanya uhalifu kwa kutumia pikipiki maarufu ‘vishandu’.

“Picha hii mjongeo iliyopo kushoto inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na watu mbalimbali kutoa maoni yao ni tukio la ukamataji lililofanywa na askari Polisi Februari 20, 2025 katika eneo la Maili Moja, Mkoa wa Pwani.

“Mtuhumiwa huyo Rajabu Hassan alikuwa anatafutwa kutokana na tuhuma mbalimbali za kujihusisha na matukio ya uporaji kwa kutumia pikipiki ikiwa imekunjwa namba za usajili (plate number) na wakati mwingine ikiwa haina namba ya usajili kwa jina maarufu Vishandu,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Hata wakati anawakimbia polisi walipojaribu kumkamata na kuwakimbia katika eneo la Mwendapole pikipiki aliyokuwa anaendesha ilikuwa haina namba ya usajili. Baadaye Polisi walipofanikiwa kukamata katika eneo la Maili Moja ilikuwa haina namba ya usajili.

“Wakati wa ukamataji alianzisha vurugu ili kukaidi ukamataji pamoja na askari kujitambulisha kwake hata hivyo walifanikiwa kumkamata na kumfikisha Kituo cha Polisi Kibaha ili kuendelea na taratibu nyingine za kisheria kuhusiana na tuhuma zinazomkabili,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Polisi imeeleza kuwa ndugu zake wanazo taarifa kuwa anashikiliwa katika kituo hicho.

Related Posts