Dar es Salaam. Serikali na kampuni binafsi zimehimizwa kuweka nyaraka zao kwenye mifumo ya kompyuta badala ya kutumia makaratasi kwa kuwa yanachelewesha utendaji wao wa kazi za kila siku.
Hayo yamebainishwa leo Februari 22, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Top Achive, Paul Mahito wakati akitoa mafunzo kwa viongozi wa sekta binafsi, wataalamu wa teknolojia na wadau wa biashara.
Lengo la mafunzo hayo ni kutoa suluhisho za kiteknolojia zinazoboresha utendaji wa biashara na kurahisisha mtiririko wa kazi katika sekta mbalimbali.
Mahito amesema kampuni hizo zikihifadhi nyaraka zao kidigitali, itawarahisishia utendaji wao wa kazi na itasaidia kupunguza gharama kutokana na karatasi wanazotumia kuhifadhi nyaraka mbalimbali na itarahisisha utendaji wao wa kazi.
“Jukwaa hili limetengenezwa kuleta mageuzi katika mashirika yanavyoshughulikia, kuhifadhi na kusimamia nyaraka zao kwa kutoa mfumo salama, wenye ufanisi na uliojaa teknolojia ya hali ya juu,” amesema na kuongeza:
“Dhamira yetu ya kuleta mabadiliko ya kidijitali nchini Tanzania na kwingineko kwa kushirikiana na kampuni ya Itiner, tunaleta suluhisho litakalowezesha biashara kusimamia nyaraka zao kwa njia rahisi, salama na endelevu,” amesema Mahito.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msimamizi wa Taasisi ya Itiner, Bela Toth amesema wanapotumia karatasi kuhifadhi nyaraka zao zinaweza kupotea au kuharibiwa, hivyo mfumo wa kidijitali unawahakikishia usalama kupitia ikiwemo njia za ukaguzi na taarifa za wakati halisi.
“Kwa zana hii ya kidijitali, biashara zitaweza kuunganishwa na wateja kwa urahisi zaidi na kupanua shughuli zao, kusaidia ukuaji wa uchumi kwa jumla,” amesema Toth.
Hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Kidijitali imewaleta pamoja viongozi wa sekta, wataalamu wa teknolojia na wadau wa biashara kushuhudia enzi mpya katika suluhisho za usimamizi wa nyaraka.
Jukwaa hilo limetengenezwa kuleta mageuzi katika mashirika yanavyoshughulikia uhifadhi na usimamizi wa nyaraka zao kwa kutoa mfumo salama, wenye ufanisi na uliojaa teknolojia ya hali ya juu.
Ubunifu huo unalingana na dhamira ya Top Archive ya kutoa suluhisho la kiteknolojia linaloboresha utendaji wa biashara na kurahisisha mtiririko wa kazi katika sekta mbalimbali.
“Uzinduzi huu ni hatua muhimu katika dhamira yetu ya kuleta mabadiliko ya kidijitali nchini Tanzania na kwingineko,” amesema Anna Chinyoyo, Mkuu wa Masoko wa Simba Money Ltd. “Kwa kushirikiana na Itiner, tunaleta suluhisho litakalowezesha biashara kusimamia nyaraka zao kwa njia rahisi, salama, na endelevu.”
Hafla hiyo imejumuisha maonyesho ya moja kwa moja, mijadala yenye maarifa kuhusu mustakabali wa usimamizi wa nyaraka na fursa za kipekee za kushirikiana na viongozi wa sekta.
Washiriki watapata uzoefu wa moja kwa moja wa uwezo wa jukwaa hili, ikiwa ni pamoja na vipengele vyake vya juu vya usalama, ujumuishaji wa wingu na otomatiki inayotumia akili bandia (AI).